Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MWAKIBETE AWAATAKA AQRB KUONGEZA USAILI WATAALAM WA MAJENGO


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, amezungumzia umuhimu wa Bodi ya Usajili Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kuongeza idadi ya wataalam wa fani hiyo waliosajiliwa nchini.

 

Akifungua mkutano mkuu wa tatu wa AQRB jijini Dar es Salaam Mhe. Mwakibete amesema Serikali itaendelea kutoa ufadhili wa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa fani hiyo kila mwaka ili kuongeza idadi ya wataalamu hao wenye sifa nchini na hivyo kuwawezesha kufanyakazi ndani na nje ya nchi.

 

" Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kwa uchumi na maendeleo ya nchi hivyo simamieni kikamilifu sekta ya majenzi ili kuboresha miji na kuleta usalama wa majengo," 

 

Mkutano huo unaoongozwa na mada kuu inayosema "uhifadhi wa majengo kwenye miji ya Afrika kwa sasa" unahudhuriwa na wataalamu mbalimbali katika sekta ya ujenzi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kuhakikisha ubunifu majengo na ukadiriaji majenzi unakwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

 

Mwakibete amewahakikishia wataalam hao kuwa  Serikali itaendelea kutoa ufadhili huo ili kuongeza idadi ya wataalamu wazawa  na kuwa katika mwaka  wa fedha 2022/23 Wizara imeidhinisha kiasi cha Shilingi milioni 550 kwa ajili ya Mpango wa Mafunzo ya Wahitimu kwa Vitendo (EAPP).

 

Naibu Waziri Mwakibete ametoa wito kwa Bodi hiyo kuziangalia upya gharama za usajili wa wanachama ili ziwe nafuu na hivyo kuwawezesha  wataalam wenye sifa kusajiliwa na kuwawazesha wananchi kutumia huduma za wataalam waliosajiliwa. 

 

Mwakibete amesema kuanzia sasa wataalamu wote watahusishwa katika miradi ya ujenzi na kwamba wizara yake imeunda timu maalumu kwa ajili ya kupitia miradi inayoendelea na kutathmini mahitaji yanayotakiwa.

 

"Kuanzia sasa lazima wataalamu wote washirikishwe kwenye miradi, Serikali itatumia wataalamu katika sekta zote ili kukidhi mahitaji ya makundi yote," amesema Mwakibete.

 

"Natoa rai kwa waendelezaji kuhakikisha wanatumia wataalamu katika miradi ya 'force account'. Serikali tunaamini kwamba force account inapunguza gharama kwa Serikali, kwa hiyo hata nyinyi hamtakiwi kutupa tofauti kubwa," amesema Mwakibete.

 

Mwenyekiti wa Bodi ya AQRB, Dkt. Ludigija Bulamile, amesema kuna umuhimu wa kushirikisha wataalamu wote katika utekelezaji wa miradi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza baada ya kukamilika kwa miradi husika.

Amesema miradi yote inatakiwa kuwa na wataalamu wote, wakiwamo wahandisi, wakandarasi na wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi ili kuzingatia mahitaji ya makundi yote yatakayotumia miundombinu.

 

Dkt. Bulamile amesema mada zitakazowasilishwa kwenye mkutano huo zitajielekeza kwenye umuhimu wa kuhifadhi majengo na kwamba majengo ya serikali yanatakiwa kuishi kuanzia miaka 60 hadi 99.

 

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Msajili wa Bodi ya AQRB, Qs. Edwin Nnunduma, amesema Bodi hiyo imesajili wataalamu 1,329, kati yao, 1,295 ni wazawa na 34 ni wageni.

 

Amesema mwaka jana waliweka lengo la kusajili miradi 1,000 lakini waliweza kusajili miradi 1,097 yenye thamani ya Sh4.5 trilioni.

 

Kuhusu wahitimu katika fani hiyo, Nnunduma amesema takribani wahitimu 250 wanahitimu masomo yao kila mwaka, lakini ni 150 pekee ndiyo wanajiunga na bodi hiyo na kupata fursa ya kupata mafunzo kwa vitendo kwenye taasisi mbalimbali za umma na binafsi.