Habari
MUST-WAIPONGEZA SERIKALI UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE MSALATO

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha sayansi na teknolojia Mbeya (MUST), wameipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa Msalato.
Spika wa Serikali ya wanafunzi wa MUST, Frank Mlay amesema ujenzi wa kiwanja hicho ni fursa kwa wasomi hasa wanafunzi wahandisi kujifunza na kupata ujuzi na hivyo kuwawezesha kuwa na maono mapana wakati wakiwa chuoni.
"Tumejifunza mengi katika ziara hii ya mafunzo na tunaomba fursa za wasomi kuja kujifunza ziwepo mara kwa mara ili kukuza uelewa wa wanafinzi kuhusu ujenzi wa miundombinu mikubwa inayoendelea nchini", amesema Mlay.
Zaidi ya wanafunzi 58 wa MUST wa kada mbalimbali za sayansi na teknolojia wameshiriki ziara hiyo.
Awali akiwakaribisha Wanafunzi hao msimamizi wa Ujenzi wa Kiwanja hicho Eng. Nziacharo Mduma amesema katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati umegawanywa katika awamu mbili ambazo ni Miundombinu ya kuruka na kutua ndege ambayo imefikia zaidi asilimia 87 na miundombinu ya majengo ya abiria na mnara wa kuongozea Ndege ambao umefikia zaidi asilimia 53.