Habari
MOROGORO: TANROADS YAFANYA TATHMINI YA BARABARA KM 2,071 NA MADARAJA 1,032 KABLA YA MVUA
Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro umeimarisha ufuatiliaji wa hali ya barabara na madaraja katika mkoa huo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa msimu wa mvua za El-Nino.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Baraka Mwambage, amesema wataalamu wa wakala huo wamefanya tathmini ya mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 2,071 pamoja na madaraja 1,032, kwa lengo la kubaini maeneo yanayohitaji uangalizi wa karibu wakati wa msimu wa mvua.
Amesema tathmini hiyo imeiwezesha TANROADS kubaini maeneo 49 yanayohitaji ufuatiliaji maalumu, hivyo kuweka mkazo katika maandalizi kulingana na hali na mahitaji ya maeneo hayo.
“Baada ya Serikali kutoa tahadhari ya El-Nino, tulifanya tathmini katika mtandao wetu wote na kubaini maeneo yanayohitaji uangalizi maalumu. Hatua hii inatusaidia kuelekeza ufuatiliaji na maandalizi yetu kwa wakati,” amesema Mhandisi Mwambage.
Ameongeza kuwa TANROADS itaendelea kufuatilia hali ya barabara, madaraja na makalavati, pamoja na kuchukua hatua za tahadhari pale inapohitajika, ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua katika miundombinu hiyo.
Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa mapema wanapoona changamoto katika barabara, madaraja au makalavati, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
