Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MOROGORO,NJOMBE, RUVUMA KUUNGANISHWA KWA LAMI 


Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Njombe -Kibena-Madeke Lupembe kuelekea Mikumi Mkoani Morogoro  ili kuunganisha Mkoa huo na mikoa ya kusini.

Akijibu swali Bungeni jijini Dodoma leo  Mhandisi Kasekenya amesema Serikali inaendelea na mpango wake wa kukamilisha ujenzi wa miradi ya barabara inayojengwa katika mikoa mbalimbali nchini.

"Mhe.Spika ujenzi wa barabara ya Mikumi-Ifakara KM 109, umekamilika,Ifakara-Mbingu KM 62. 5  na Mbingu-Chita KM 37.7 ujenzi unaendelea, Chita-Kibena mkoa wa Njombe Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi"Amesema Mhandisi Kasekenya

Aidha Naibu Waziri alikua akijibu swali la Mhe. Mbunge Viti Maalum Neema Mgaya  aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Njombe-Kibena-Madeke-Lupembe  mkoani Morogoro.

Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara sehemu ya Ifakara-Lupilo-Mtimbila KM 112  kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa sanifu jenga.

Barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kidatu-Ifakara- Londo hadi Lumecha Mkoani Ruvuma yenye jumla ya urefu wa km 435.8