Habari
MIUNDOMBINU YA BARABARA SIMIYU YACHOCHEA UCHUMI NA USAFIRI
Miundombinu bora ya barabara na madaraja imeendelea kuwa sehemu muhimu ya kuchochea shughuli za kiuchumi na kurahisisha maisha ya wananchi katika Mkoa wa Simiyu, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu hiyo.
Akizungumza kuhusu mchango wa miundombinu katika maendeleo ya Mkoa wa Simiyu, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Boniface Mkumbo, amesema uwepo wa mtandao wa barabara za lami umeongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji, hususan kwa mazao ya kilimo, mifugo na bidhaa mbalimbali.
Amesema Simiyu ina mtandao wa barabara kuu mbili za lami zinazoiunganisha na mikoa ya Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Kati, zikiwemo barabara ya Mwanza–Mara yenye urefu wa kilomita 58.6 inayopita Mkoa wa Simiyu na barabara ya Lamadi–Bariadi–Maswa–Shinyanga yenye urefu wa kilomita 155.
“Miundombinu hii imekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa, pamoja na kuwawezesha wananchi kufikia huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa urahisi zaidi,” amesema Mhandisi Mkumbo.
Kwa upande wa madaraja, amesema TANROADS imejenga Daraja la Sibiti lenye urefu wa mita 160, lililopo katika barabara ya Bariadi–Mwangongo–Mwanhuzi–Sibiti–Singida, ambalo limeongeza ufanisi wa mawasiliano ya barabara kati ya Simiyu na maeneo mengine ya nchi.
Ameeleza kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuboresha usalama na mazingira ya usafiri mijini, ambapo jumla ya taa 800 za barabarani zimewekwa katika miji na vituo mbalimbali, zikiwemo taa za kuongozea magari katika makutano ya barabara.
Mhandisi Mkumbo amesema taa hizo zinapatikana pia katika maeneo muhimu kama Makao Makuu ya Mkoa mjini Bariadi na Wilaya ya Maswa, hatua inayolenga kuimarisha matumizi salama ya barabara, hususan wakati wa usiku.
Aidha, amesema TANROADS imejenga maeneo mawili ya mapumziko katika Mji wa Bariadi pamoja na maeneo mawili ya maegesho ya magari, kwa lengo la kuboresha mazingira ya wasafiri na watumiaji wengine wa barabara.
Katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya Serikali, amesema TANROADS pia imeweka mabango ya kidijitali katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutoa taarifa kuhusu miradi ya kitaifa inayotekelezwa katika Mkoa wa Simiyu.
Kwa ujumla, uwekezaji huo unaendelea kuifanya miundombinu ya barabara kuwa nyenzo muhimu katika kuunganisha wananchi, masoko na huduma, huku ukifungua fursa zaidi za shughuli za kiuchumi na kijamii ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu.
