Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MIKAKATI YA RAIS SAMIA KUINUA MAKANDARASI WAZAWA.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka kuona ushiriki mkubwa zaidi wa Makandarasi wazawa katika kazi za utekelezaji wa ujenzi wa miradi nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa leo tarehe 21 Novemba, 2023 katika Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi na Washauri elekezi wa ndani jijijini Dodoma, kujadili nafasi yao katika utekelezaji wa miradi.

Bashungwa amesema Wizara ya Ujenzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea kutenga miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa ajili ya makandarasi wa ndani kwa lengo la kuwasaidia makandarasi hao kukua na kupata uzoefu.

“Katika mwaka wa fedha 2023/204, jumla ya miradi minne ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 kila moja zimetengwa kwa ajili ya makandarasi wa ndani tu, kwa hiyo kilometa 200 zitajengwa na wazawa, hii ni fursa kubwa ya kuwasaidia makadarasi”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesisitiza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Jumla ya kilometa 20 za barabara zimetengwa kwa ajili ya makandarasi wanawake, ambapo zitagawanywa katika vipande vya kilometa tano tano, na kazi hizo zitashindanishwa kwa makampuni ya wanawake peke yao, hii inafanya jumla ya km 220 kujengwa na makandarasi wazawa kwa mwaka 2023/24.

Bashungwa ameongeza kuwa kazi za matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara zenye thamani ya Shilingi Bilioni 600 zitatekelezwa na Makandarasi wa ndani tu katika mikoa yote 26 nchini.

“Katika Mwaka wa fedha 2023/2024 kazi zote za matengenezo ya barabara kwa mikoa yote 26 nchini, Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kutekelezwa na Makadarasi wa ndani”, amesema Bashungwa.

Halikadhalika, Bashungwa amefafanua kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma imefanyiwa marekebisho kwa kuongeza kiwango cha thamani ya mradi ambao utatekelezwa na Makandarasi wa ndani tu, bila kushindanishwa na Makandarasi wa nje.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka makandarasi kuchangamkia fursa ambayo Rais Samia ametoa kwa makandarasi wa ndani na kuacha kudharauliana ili kupata maendeleo kwao na Taifa kwa ujumla.

Dkt. Nchemba, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuongeza fedha   kila mwezi kwa Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS ili iweze kuongeza kasi ya kulipa madeni ya makandarasi wazawa.

Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema kuwa kwenye ilani ya Chama hicho imeahidi kuhakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa makandarasi wa ndani na kuwasisitiza kufanya kazi kazi kulingana na miiko ya taaluma yao.

Dhima kuu ya mkutano huu ni kujadili na kudadavua mikakati mbalimbali kati ya Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi kuhusu kuwajengea uwezo makandarasi wazawa na washauri elekezi.