Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MIGIRE AAGIZA TPA KUANZA KUTOA HUDUMA BANDARI YA KWALA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi anayesimamia Sekta ya Uchukuzi Bw.Gabriel Migire, amewaagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) kwa kushirikiana na Taasisi  nyingine za Serikali na Binafsi  kuhakikisha  Bandari kavu ya Kwala inaanza kazi.

Migire ameyasema hayo kwenye Mkutano wa Maboresho ya Bandari ya Dar es salaam ambao umewakutanisha Uongozi wa Usimamizi wa Bandari (TPA), Wizara na wadau mbalimbali wanaotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Bandari Kavu ya Kwala inatakiwa kuanza kazi haraka ili kupunguza msongamano wa shehena na Magari makubwa katika Bandari ya Dar es Salaama” alisema Migire.

Aidha, Migire aliongeza kuwa kukamilika kwa Bandari kavu ya Kwala kutasiadia kupunguza foleni ya magari makubwa katika jiji la Dar es Salaam, hivyo aliitaka kila taasisi ifanye wajibu wake ili bandari hiyo ianze kufanya kazi.

Kwa upande wake Meneja wa Bandari Kavu ya Kwala, Alexander Ndibalema, amesema kuwa ujenzi wa Bandari hiyo umefikia asilimia 90 na unatarajia kukamilika mwishoni mwa Mwezi Machi 2023, pia ujenzi wa Barabara ya Zege ya zaidi ya kilometa kumi na tano kutoka Vigwaza mpaka Bandari kavu ya Kwala imekamika.

Halikadhalika Ndibalema alifafanua kuwa Mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam itasafirishwa kwa treni mpaka Kwala hivyo anatarajia mizigo kwenda nje ya Tanzania na ndani ya Tanzania yote itachukuliwa katika Bandari hiyo.

Katika hatua nyingine Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho, amesema kuwa kwa sasa katika bandari ya Dar es Salaam Shehena imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 22 hivyo kutoa wito kwa kila mdau kuhakikisha anawahi kuhamisha mizigo hasa mizigo ya taasisi za Serikali ambayo inakaa baharini hapo kwa Muda mrefu.