Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MBARAWA AAGIZA UBORA WA JENGO LA ABIRIA KIWANJA CHA NDEGE CHA ARUSHA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), kuhakikisha jengo la abiria linalojengwa katika Kiwanja cha Ndege cha Arusha linakamilika kwa kukidhidhi viwango vya Kimataifa.

 Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo hilo, Mkoani Arusha, Profesa Mbarawa amesema kiwanja hicho kinatumiwa zaidi na watalii hivyo ni muhimu wataalam wakazingatia uwepo wa miundombinu wezeshi na inayovutia ili kushawishi mashirika mengi zaidi ya ndege kukitumia.

“Asilimia kubwa ya abiria wanaotumia kiwanja hiki ni wageni ambao ni watalii, hivyo hakikisheni jengo linakamilika kwa kuweka vitu vitakavyovutia zaidi ili kuruhusu ongezeko la abiria na ndege sababu tuna fursa ya kuwa na vivutio vingi vya utalii mjini hapa”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amesema pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka katika maboresho ya Viwanja nchini amewataka kuhakikisha maboresho hayo yanakwenda sawa sawa na ongezeko la mapato ili nyongeza hiyo itumike katika kuboresha kiwanja hicho kwa kukiwekea taa ili kitumike saa 24.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo ameipongeza Serikali kwa kuboresha jengo la abiria kwani imekuwa changamoto ya muda mrefu ambapo kukamilika kwake kutapunguza usumbufu kwa abiria wanaotumia kiwanja hicho.

Naye Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Arusha, Eng. Elipid Tesha, amemueleza Waziri kuwa mradi huo utaongeza mapato ya Kiwanja kutoka Bilioni 2.8 hadi kufikia bilioni 6 kwa mwaka.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutaruhusu kuhudumia abiria laki tano hadi sita kwa mwaka ambapo kwa sasa jengo lililopo linahudumia abiria laki mbili tu kwa mwaka.

Aidha, Eng. Tesha amemuhakikishia Waziri Prof Mbarawa kuwa TAA itakamilisha jengo hilo kwa kuzingatia thamani ya fedha na ubora.

Jengo la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Arusha linagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.8 na limeshafikia asilimia 75 na linatarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.