Habari
MAKANDARASI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA VIWANGO STAHIKI.

Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Eng. Rhoben Nkori, ametoa wito kwa Makandarasi nchini kutekeleza miradi kwa viwango stahiki ili watanzania waweze kunufaika na miradi hiyo.
Ameyasema hayo katika mafunzo ya kuwajengea uwezo makandarasi, yanayotolewa na Bodi ya Makandarasi (CRB) chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi yaliyofanyika jijini Dodoma.
“Ukandarasi ni biashara kubwa, ni biashara muhimu kwa nchi, inategemea miundombinu ya nchi kwa hiyo makandarasi wanapoaminiwa kupewa miradi ni lazima watekeleze miradi kwa kiwango kinachostahili, kwa muda unaostahili na kwa gharama inayostahili ili watanzania waweze kunufaika na miundombinu inayojengwa”, amesema Msajili.
Kwa upande wake, Eng, Joan Agustino Peter Meneja wa kampuni ya JOMEFA Investiment iliyopo Dodoma, mmoja wa makandarasi aliyehudhuria mafunzo hayo, ameiahidi serikali kufanya kazi vizuri kutokana na kiu waliyonayo ya kuwa wakandarasi wakubwa ili waweze kupata miradi mikubwa, kupitia mafuzo waliyoyapata.
Naye, Eng. Yahaya Mnali, mmiliki wa kampuni ya ujenzi ya Salehe Msahala Contractor Limited iliyopo Dar es salaam, ameeleza manufaa wanayoyapata kutokana na mafuzo hayo ikiwemo kujijengea uwezo wa kufanya miradi mikubwa kutokana na mahusiano baina ya wakandarasi wadogo na wenye uwezo mkubwa na serikali kuiahidi Serikali kufanya kazi kitaalamu na kwa ubora wa hali ya juu.