Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KIWANJA CHA NDEGE IRINGA KUKAMILIKA AGOSTI


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya kiwanja cha ndege cha Iringa utakamilika ifikapo Agosti mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa kiwanja hicho mjini Iringa Profesa Mbarawa  amesema kiasi cha shilingi bilioni 63.7 kilichotengwa kitakamilisha ujenzi huo na kuondoa kero ya muda mrefu kwa wakazi wa mkoa wa Iringa katika kupata huduma za uhakika za ndege.

“Hadi sasa tumefika asilimia 45 za ujenzi na sehemu iliyobaki tutaikamilisha ifikapo Agosti mwaka huu”, amesema Waziri Profesa Mbarawa.

Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa  kuanzia Agosti ndege kubwa  zitatua katika kiwanja hicho usiku na mchana na zitakuwa zikibeba abiria wengi hivyo kuwataka wakazi wa mkoa wa huo na Njombe  kujipanga kuhudumia wataii wengi wanaokwenda katika mbuga ya Taifa ya Ruaha na hivyo kupata manufaa.

Kwa upande wake Mbunge wa Isimani Mhe. William Lukuvi ameishukuru Serikali kwa namna inavyojenga miundombunu mkoani Iringa na kusisitiza kuwa kiwanja cha ndege cha Iringa kitakuwa ufunguo wa utalii na fursa za ajira mkoani humo.

Naye meneja wa Wakala wa Barabara mkoani Iringa eng. Daniel kindole amesema ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa unaenda sambamba na uboreshaji wa barabara ya Mchepuo Km 7, na Serikali imepanga kujenga barabara ya Mafinga- Mgololo (Km 80) kwa kiwango cha lami ili kukuza uchumi wa wananchi katika maeneo ya uzalishaji.