Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KIWANJA CHA NDEGE CHA TABORA KIKAMILIKE KWA WAKATI


Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Tabora kuhakikisha wanasimamia ipasavyo ukarabati na uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Tabora ili kikamilike.

Kasekenya ameyasema hayo mara baada ya kukagua kiwanja hicho na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wake, ambapo mradi huu unatakiwa kukamilika ifikapo Machi, 2024.
“Kwenye huu mradi kusiwe na vikwazo vyovyote ambavyo vitapelekea kazi kusimama, kama mvua zinanyesha basi hakikisheni mnawasimamia wanafanya ili kazi ambazo haziathiriwi na mvua ndizo zifanyike,“ amesema Kasekenya.

Vile vile amesisitiza kwa wakandarasi wasiomaliza kazi kwa wakati wawajibishwe kwani hakuna haja ya kuchelewesha mradi ikiwa gharama za awali zimeshalipwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi anayesimamia mradi huo, Eng. Vicent Aron amesema kwa kuzingatia shughuli zote ambazo zimefanyika kwenye ujenzi, mradi kwa sasa umefika asilimia 12.9 dhidi ya maendeleo yaliyopangwa ya asilimia 13 kwa kuzingatia siku 75 zilizotumika.

Aidha, ameongeza  kuwa wameongeza jitihada za kumsimamia Mkandarasi M/S BEIJING CONSTRUCTION ENGINEERING GROUP CO.LTD, katika kuhakikisha anamaliza kazi kwa wakati kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi, kuongeza muda wa kufanya kazi siku zote za wiki na sikukuu za kimataifa.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara  Nchini (TANRODAS) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Raphael Mlimaji amemuhakikishia Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya kusimamia kiwanja cha ndege hicho kwa ukaribu na kuhakikisha kinakamilika kwa muda ulipangwa.
 

Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi, Dkt. Batlida Salha Burian, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Ujenzi, kwa uboreshaji wa Kiwanja cha ndege, kwani kukamilika kwake kutatochechea shughuli za kiuchumi na kimaendeleo katika mkoa huo.

Vilevile, ameomba Jitihada za Ujenzi wa Barabara ya Ikole hadi Rungwa ziendelee kwani ni Barabara muhimu inayounganisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nyanda za juu kusini.