Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Kasekenya: TANROADS ongezeni kasi upimaji uzito wa magari


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuongeza kasi ya upimaji wa magari yanayopita kwenye mizani zote nchini ili kupunguza malalamiko kwa wasafirishaji.

Ameyasema hayo jijini Arusha, wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mizani mipya na ya kisasa ya Kimokouwa iliyopo wilayani Longido ambayo itatumika kwa ajili ya kupima uzito wa magari yanayofanya safari zake kati ya Tanzania na nchi jirani ya Kenya.

“Nitoe rai kwa wasafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizi mbili kutozidisha uzito wa magari yenu pindi mnapotumia barabara zetu, kwani kwa kufanya hivyo mnaharibu miundombinu ya barabara hizi ambazo Serikali imetumia fedha nyingi kuzijenga,” amesema Kasekenya.

Ameongeza kuwa kama wasafirishaji wote watasafirisha bidhaa zao bila kuzidisha uzito miundombinu ya barabara nchini itakuwa imelindwa na kuzifanya barabara zote nchini kudumu kwa muda mrefu bila kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Mhandisi Kasekenya ameutaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoani Arusha, kuhakikisha wanaendelea kusimamia kikamilifu mradi huo wa ujenzi wa mizani ya Kimokouwa ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vilivyokubaliwa kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wake.

Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amesema mradi wa ujenzi wa mizani ya Kimokouwa unaotekelezwa na Kampuni ya CRJE (EAST AFRICA) LTD, unagharimu Shilingi za Kitanzania Bilioni 14 zinazotolewa na Serikali ya Tanzania ambapo kwasasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 89 na unatarajia kukamilika mapema ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Kwa upande wake Mhandisi Mshauri kutoka kampuni ya Ambicon Engineering, Eng. Samweli Mtawa, amesema kuwa kazi zilizokwishafanyika hadi sasa ni pamoja ujenzi wa barabara za maingilio kilometa 1.1, ujenzi wa sehemu za kukagulia magari, ujenzi wa maeneo mawili ya kuegeshea magari, ujenzi wa majengo ya ofisi, walinzi pamoja na vyoo, ujenzi wa nyumba kwa ajili ya watumishi na uzio ambazo ni kazi za nyongeza unaendelea.

Mhandisi Kasekenya yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali inayosimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi