Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA; HAKUNA MRADI WA UJENZI UTAKAOSIMAMA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema hakuna mradi wa ujenzi utakaosimama katika awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chote cha mwaka.

Kasekenya ameyasema hayo leo  baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Kibaoni-Sitalike ( Km 74) inayojengwa kwa kiwango cha lami, kipande cha kwanza cha Kibaoni -Makutano ya Mlele (Km 50) kinachojengwa na Mkandarasi M/S China Railway Seventh Group Co.Ltd (CRSG), mkoani Katavi.

“TANRODS Hakikisheni mnasimamia miradi ipasavyo, hakuna mradi ambao utasimama kwa uzembe wa Mkandarasi kwani Serikali imeshatoa fedha kazi ziendelee kufanyika kipindi chote cha mwaka” amesema Kasekenya .

Kasekenya  amemtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi ili barabara hiyo ikamilike kwa wakati kama ilivyopangwa kwenye mkataba .

“Mpo nyuma sana kwenye ujenzi, na hakuna sababu yoyote ya msingi, na msitegemee kama tutatoa muda wa Ziada na mlichoahidi kwa Serikali kitekelezwe” amesisitiza Kasekenya

Kwa Upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi, Mhandisi Martin Mwakabende amesema kuwa ujenzi wa Barabara hiyo unaanzia Kibaoni hadi makutano ya Mlele yaliyopo katika mbuga ya Wanyama ya Katavi ( Katavi National Park).

Aidha, amesema kuwa  Ujenzi huo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 na unatarajia kukamilika June 2025.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amewapongeza Wakala wa Barabara Nchini ( TANROADS) kwa kuendelea kusimamia vyema ujenzi wa daraja  la Kavuu  lililopo mkoani Katavi lenye urefu wa mita 87.5  linalojengwa na Mhandisi/s NGETIJO GROUP CO.LTD ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 57.

Naibu Waziri huyo, amemsisitiza Mkandarasi kutembelea site mara kwa mara ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa ubora na kukamilika kwa wakati.

Halikadhalika,  amewaagiza TANROADS kuhakikisha wanaweka kiwango thabiti cha uzito wa magari yanayobeba  mizigo kwani daraja hilo ni muhimu sana na ni kiunganishi cha Mkoa wa Tabora,Katavi,Rukwa na Songwe.