Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

KASEKENYA AWAASA WADAU WA UJENZI DAR


NAIBU Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa wadau wa ujenzi nchini kutumia kikamiifu fursa zinazotolewa na Serikali katika kuwawezesha kukua kitaaluma na kiuchumi ili kuwaletea maendeleo.

Akizungumza wakati akifungua maonesho ya saba ya wadau wa ujenzi jijini Dar es Salaam, Eng. Kasekenya amewataka wadau hao kutafuta ufumbuzi utakao wawezesha kuungana na kunufaika na miradi mingi ya ujenzi inayoendelea nchini.

“Hakikisheni kazi mnazopewa na Serikali mnazifanya kwa ubunifu na kuzikamilisha kwa wakati ili kuiwesha Serikali kuwaamini na kuwapa miradi mingi zaidi na hivyo kuwapa fursa ya ajira na kukuza uchumi wa watanzania.

Naibu Waziri huyo amesema zaidi ya kilomita 25 elfu za barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), ambazo ni za changarawe zinahitajika kujengwa kwa kiwango cha lami na takriban nyumba laki mbili zinahitajika kujengwa nchini kila mwaka hivyo kufanya wadau wa sekta ya ujenzi kuwa na kazi kubwa ya kufanya.

Maonesho hayo ya saba ya wadau wa ujenzi mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “ujenzi wa siku zijazo ubunifu wa miji ya kisasa”.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng. Menye Manga amezungumzia umuhimu wa wadau wote wa ujenzi kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa nchini inalinda mazingira.

“Maendeleo ya Ujenzi wa miundombini na viwanda yatafikiwa kwa haraka endapo ujenzi wake utaendana na utunzaji wa mazingira kwa maslahi ya miji endelevu,” amesisitiza Eng. Manga.

Mtendaji Mkuu wa maonesho hayo Bw. Deogratias Kilawe amesema maonesho ya mwaka huu yataleta chachu ya kuwavuta wadau wengi kuwekeza kwenye sekta ya ujenzi na hivyo kuchangia pato la Taifa.