Habari
KASEKENYA AAGIZA UWANJA WA NDEGE WA SUMBAWANGA UKAMILIKE KWA WAKATI
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amemtaka Mkandarasi kampuni ya M/S Beijing Construction Engineering group kuongeza kasi ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga ili uweze kukamilika mapema iwezekanavyo.
Mhandisi Kasekenya, ametoa agizo hilo tarehe 8 Januari, 2025 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo ambao umefikia asilimia 40 Wilayani Sumbawanga Mkoani Rukwa.
“Nitoe maelekezo kwa wanaosimamia na kutekeleza mradi huu ambao ni TANROADS, Mhandisi Mshauri pamoja na Mkandarasi kuhakikisha vifaa vyote muhimu vinafika site kwa wakati ili kuendana na kasi na muda uliopangwa kukamilika kwa uwanja huu”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya amesema Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga ni mojawapo ya miradi ya viwanja vya ndege vinne ambavyo vinajengwa kwa ushirikiano na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya vikiwemo na Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Shinyanga na Tabora.
Aidha, Mhandisi Kasekenya ameeleza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutaongeza fursa za uwekezaji kutoka Mikoa na Nchi jirani kuweza kufika na kuwekeza Mkoani humo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uwanja wa ndege kutoka TANROADS Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Samweli Buha ameeleza kuwa uwanja wa ndege huo umefikia asilimia 40 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Machi 2025.
Ameongeza kuwa hadi hivi sasa ujenzi wa jengo la abiria pamoja na barabara za maingilio zimefikia asilimia 90 na kazi zinazoendelea kufanywa na Mkandarasi ni ujenzi wa tabaka la juu la msingi wa kati, ujenzi wa tabaka la chini katika barabara ya kuruka na kutua ndege.