Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

DKT. SAMIA ATOA BILIONI 254 NDANI YA MIEZI MIWILI KULIPA MAKANDARASI WA BARABARA NA MADARAJA


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sitainayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa takribani Sh bilioni 254 ndani ya miezi miwili, kwa ajili ya kulipa Makandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya barabara na madaraja nchini na kueleza kuwa kazi hiyo ya kuwalipa Makandarasi bado inaendelea.

Amesema hayo jijini Dodoma mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Ntyuka hadi Kikombo yenye urefu wa kilomita 76 inayojengwa kwa awamu mbili na wakandarasi wawili ambao ni CHICO pamoja na China First.

Aidha, Ulega amesema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais  Samia ni kuhakikisha kuwa miradi yote ya Sekta ya Ujenzi iliyosimama inaendelea kutekelezwa  kama ilivyopangwa na tayari Serikali imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.

“Mmeona katika muda wa hii  miezi mwili, Rais Samia tayari amelipa malipo ya wakandarasi ya takribani shilingi bilioni 254, matumaini yetu  tunataka kuona kazi zikiendelea “, amesema Ulega.

Kadhalika,  Ulega amemhakikishia Mkandarasi CHICO kuwa atalipwa  malipo anayodai katika barabara hiyo na hivyo kumtaka arudi eneo la ujenzi na kuendelea na kazi usiku na mchana ili ikamilike kwa wakati na wananchi kuweza kunufaika na fursa ya uwepo wa barabara hiyo.

“Tumekubaliana tunakwenda kukaa na timu ya mkandarasi  pamoja na wataalamu wangu kutoka Wizarani ili kuhakikisha tunaliweka sawa suala hili la malipo”, amesisitiza Ulega.

Ulega ameongeza kuwa mwishoni mwa Februari mwaka huu, Serikali inatarajia kutoa fedha nyingine za kutekeleza miradi ya miundombinu katika Sekta ya ujenzi ambapo ameiagiza TANROADS kuipa kipaumbele barabara hiyo ili ianze kujengwa haraka.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini na Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema kuwa barabara ya Ntyuka - Mvumi- Kikombo ni barabara ya kihistoria hivyo ameomba Serikali kukamilisha barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani ni mkombozi kutokana na  uwepo wa hospitali kubwa ya macho ya MVUMI  inayotoa huduma nchi nzima na pia  kuunganisha maeneo mbalimbali ya jiji hilo.

 Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Dodoma,  amaipongeza Serikali  ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa barabara hiyo kwani mradi  huo tayari umenufaisha wananchi 201 kwa kutoa ajira za muda hadi sasa.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi, Mohammed Besta amesema kuwa Ujenzi wa barabara ya Ntyuka - Mvumi- Kikombo unatekelezwa kwa Sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza kutoka  Ntyuka- Mvumi-  Makulu na Kikombo - Chololo  -Mapinduzi (Km 25) inatekelezwa na Mkandarasi CHICO  kwa gharama ya shilingi Bilioni 38.1 na sehemu ya Pili ya Ntyuka  -Mvumi Hospitali - Kikombo (Km 53) inatekelezwa na Mkandarasi China First kwa gharama ya Shilingi Bilioni 98.4.