Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

DKT. MSONDE ARIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA DHARURA DODOMA.


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dkt Charles Msonde amempongeza Mkandarasi M/S Andic Limited kwa utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Morena ambalo kwa sasa limefika asilimia 80.

Pongezi hizo amezitoa Mei 12, 2025 jijini Dodoma alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya dharura ambapo ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

“Nimefurahishwa na utekelezaji wa mradi huu, hakikisheni mnamsimamia mkandarasi ili amalize kazi kwa ubora na kwa wakati”, amesema Naibu Katibu Mkuu.

Aidha, Dkt. Msonde amekagua mradi wa ujenzi wa Daraja la Mbande ambapo amemtaka Mkandarasi wa mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi kwa wakati.

Dkt. Msonde, ameupongeza Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kusimamia vyema matumizi ya fedha za miradi ya dharura ambayo ilipata athari kutokana na mvua za El-Nino zilizonyesha nchini.

“Serikali ilitoa zaidi ya shilingi Billioni 866 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya dharura, hivyo matarajio makubwa ya Serikali ni kuhakikisha kazi za ujenzi wa Madaraja zinafanyika usiku na mchana Ili kukamilika", amesema Dkt. Msonde.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani amesema kuwa mradi wa Daraja la Morena unatekelezwa na mkandarasi mzawa na unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 1.5.

Mhandisi Amani ameeleza pia ujenzi wa daraja la Mbande unaotekelezwa  na mkandarasi King's Builders kwa gharama ya shilingi Bilioni 7 umefika asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2025.

Kuhusu utekelezaji wa Mradi wa dharura katika Daraja la Nzare, Mhandisi Amani amesema kuwa mradi huo unatekelezwa na mkandarasi CHICO na kusimamiwa na TECU Mkoa wa Doodoma ambao unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 14.5 ambapo kazi zinazofanyika sasa ni uchimbaji wa nguzo na matengenezo ya Barabara za maingilio.