Habari
DKT. MPANGO AWEKA JIWE LA MSINGI SGR TABORA-ISAKA

akamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema Serikali itaendelea kuhakikisha miradi yote ya kimkakati ya ujenzi wa miundombinu inaendelezwa na kukamilika ili kuchochea uchumi.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, kipande cha nne sehemu ya Tabora hadi Isaka kilomita 165 Dkt. Mpango ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha inasimamia vizuri mradi huo na kudhibiti mfumuko wa gharama.
“Hakikisheni wakazi wa Mkoa wa Tabora na Shinyanga wanapata ajira na wanafanya kazi kwa ubunifu, uzalendo na kujituma”, amesema Dkt. Mpango.
Aidha ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha ujenzi wa reli ya SGR unaendana na ujenzi wa Chuo cha Reli Tabora kitakachowezesha kuandaa wataalam watakaohudumia reli hiyo ili iwe endelevu.
“Waziri fuatilia fursa za ajira kwa wataalam wetu ziwe nyingi ili kuwawezesha kuufahamu mradi kikamilifu na kuuendeleza pindi wakandarasi watakapokamilisha ujenzi.
Amemtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha wakandarasi wadogo wanaofanya kazi kweye mradi huo wanalipwa madai yao kwa wakati na kuonya wafanyakazi wanaoiba mafuta na vifaa vya mkandarasi kuwa hatua kali za kisheria zichukuliwe ili kuthibiti uhujumu uchumi.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemhakikishia Makamu wa Rais Dkt Mpango kuwa Wizara imejipanga kikamilifu kusimamia kwa ukamilifu mradi huo kwa kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza na Tabora hadi Kigoma ili kuiungaisha Tanzania na Nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda na Rwanda na hivyo kukuza uchumi wa Tanzania kupitia nchi za maziwa Makuu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kuanza kwa ujenzi wa reli katika kipande cha Tabora hadi Isaka kunakamilisha ujenzi wa reli hiyo sehemu ya Dar es Salaam hadi Mwanza KM 1596 na mipango kwa ajili ya kupokea mabehewa na injini za reli hiyo iko katika hatua nzuri.
Zaidi ya shilingi trillioni 23.3 zinatarajiwa kutumika katika mradi wote wa reli ya SGR hapa nchini.