Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

CAG KICHERE AIPA HEKO TANROADS UJENZI UWANJA WA NDEGE MSALATO


Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Charles Kichere amepongeza kasi ya ujenzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato wenye ukubwa wa hekta 4,500( hekari 11000).

CAG Kichere ametoa pongezi hizo leo tarehe 4 Februari 2025 wakati alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja cha ndege wa Msalato Jijini Dodoma.

“Tumeona ni bora kuja eneo la mradi ili kujionea utekelezaji wake kuliko kukaa ofisini tu na kusoma ripoti, nitoe pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita inaayoongozwa na na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu”, amesema Kichere.

Aidha, Kichere amehimiza wakandarasi wa mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati unaotakiwa na kutoa wito kwa wananchi kutovamia maeneo hayo ya uwanja kwani ni alama ya mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla wake.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi, Mohamed Besta amesema kuwa uwanja huu utakamilika rasmi mwezi Novemba 2025 na kuanza kutumika ifikapo Julai 2025.

Mhandisi Besta amesisitiza kuwa wananchi wanautazama uwanja huo kama sehemu ya uwekezaji nchini hivyo kasi ya ujenzi itaendelea ili ukamilike kwa wakati.

Naye Msimamizi wa mradi, Mhandisi Kendrick Chawe amesema kuwa uwezo wa uwanja huo kiteknolojia na ufanisi wa maegesho ya ndege una uwezo wa kuchukua ndege 17 kwa wakati mmoja.

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato utakuwa kiungo muhimu cha usafiri wa anga nchini Tanzania, Afrika Mashariki na Ulimwengu kwa ujumla wake ambao utachochea maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa pindi utakapokamilika.