Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BILIONI 70 ZATENGWA KULIPA MADENI YA MAKANDARASI KILA MWEZI


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga shilingi Bilioni 70 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi wanaoendelea kutekeleza miradi ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo Bilioni 50 zinaenda kulipa makandarasi wa ndani na Bilioni 20 kwa makandarasi wa nje.

Amesema hayo wakati akikagua utekelezaji wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa ambao ujenzi wake umefikia hatua za mwisho na unatarajiwa kukabidhiwa kwa wana Iringa mwishoni mwa mwezi huu.

“Mheshimiwa Rais ameiwezesha Wizara ya Ujenzi kwa kutupa Bilioni 70 kwa ajili ya kulipa makandarasi wa ndani kama kipaumbele cha kwanza kwa madeni ambayo wamekuwa wakidai hadi Juni 30, 2023”, amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa kwa utaratibu huo ndani ya miezi mitatu na nusu Serikali itakuwa imekamilisha madeni ya makandarasi wa ndani ili kazi zote zilizokuwa zikifanywa na makandarasi hao zisiweze kusimama, baada ya hapo fedha hizo (bil 70) zitaendelea kulipa madeni yaliyobaki kwa wakandarasi wa nje.

Bashungwa amesema kuwa mbali na Serikali kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja ya kimkakati juhudi hizo zinaenda sambamba na kujenga anga la Tanzania ili kuimarisha usafiri wa anga kwa kuboresha viwanja vya ndege nchini.

Kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Iringa, Waziri Bashungwa amesema ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais kukamilisha kiwanja hicho kwa viwango vya juu ili kuruhusu ndege kuruka na kutua saa 24.

“Wana Iringa niwapongeze sana kwa kupata uwanja, uwanja ambao sasa hivi hata wawekezaji wanaotaka kuwekeza Iringa watakuwa na uhakika kuna uwanja ambao umezingatia mambo yote ya kiusalama”, amefafanua Bashungwa.

Sambamba na hilo, Waziri Bashungwa amesema kuwa Mhe, Rais ameelekeza Ujenzi wa barabara ya mchepuo (Iringa Bypass) yenye urefu wa kilometa 7.3 ili ya kuondokana na adha ya wana Iringa kuingia na kutoka katikati ya mji.

“Mhe. Rais mambo ya mchakato hataki kuyasikia, anataka mkandarasi apatikane hivyo mkandarasi aliyetekeleza ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Iringa ndiye  huyo atakeyejenga na barabara hii”, amesisitiza Bashungwa.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mha. Mohamed Besta amesema kuwa kiwanja hicho kinatekelezwa na mkandarasi Sinohydro kwa gharama ya Shilingi Bilioni 63.7 ambapo kitakuwa na uwezo wa kupokea ndege za kati kama Bombardier kwani kitakuwa na urefu wa mita 2100 na upana wa mita 30.

Kukamilika kwa kiwanja hicho kutakuwa na huduma muhimu kama vile sehemu ya zimamoto, pamoja na eneo maalum la kufua umeme na jengo la kusaidia umeme pale unapozimika na kufanya kiwanja hicho kuwa na umeme wa kuaminika masaa yote.
Kiwanja cha Ndege cha Iringa ni miongoni mwa viwanja vya ndege 11 nchini vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kati ya mwaka 2014 hadi 2017 ambapo hapo awali kilianza kutumika mwaka 1950 huku miundombinu yake ilijengwa kati ya mwaka 1970 hadi 1980.