Habari
BILIONI 113 KUJENGA KM 50 BARABARA YA ZEGE KUELEKEA LIGANGA NA MCHUCHUMA.
Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa barabara ya Itoni-Lusitu (km 50) kwa kiwango cha zege, ambayo itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 113 ili kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya Chuma cha Liganga.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa Wilayani Ludewa mara baada ya kukagua barabara hiyo pamoja na kipande cha Lusitu-Mawengi (km 50) kilichokamilika kwa kujengwa kiwango cha zege na Wananchi tayari wameshaanza kunufaika nayo.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana mkakati maalumu na mkoa huu wa Njombe kwa kuwa fedha hizi zote zinawekwa hapa ili kuufungua Wilaya ya Ludewa kibiashara”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amesema uwekezaji unaowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika mkoa huo utafungua fursa ya kupitisha madini ya chuma kutoka Liganga-Mchuchuma hadi kufika Njombe na mikoa mingine.
“Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifungua mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujenzi wa barabara za lami na zege ili kuweza kuuruhusu uchumi uliofungwa kwa muda mrefu kamma ilivyokuwa kwenye mradi wa liganga-mchuchuma ulivyokaa zaidi ya miaka 40” amesisitiza Bashungwa.
Vilevile, Bashungwa amemtaka Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa barabara Itoni – Lusitu (km 50), Cheil Engineering Co. ltd kumsimamia kwa karibu mkandarasi China Civil Engineering Construction Cooperation ili aweze kukamilisha mradi huo kama mkataba unavyosema amalize Disemba 2024.
Ameongeza kuwa barabara hiyo ni kiunganishi cha nchi za Malawi na Tanzania upande wa Nyanda za Juu Kusini ambapo ikikamilika itachochea ukuaji wa uchumi na kuwa kiungo kizuri kati ya mgodi wa makaa ya mawe (mchuchuma) Bandari za Dar es salaam, Tanga na Mombasa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa bilioni 15 kwa kulipa fidia wananchi waliopisha miradi hiyo ya mchuchuma na liganga.
Ameeleza barabara hiyo itaongeza pato la Taifa kutokana na shughuli za kiuchumi kama uchimbaji wa makaa ya mawe na usafirishaji wa mazao ya misitu kutoka mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma kwenda nchi jirani na mikoa jirani ya Tanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Njombe ambaye pia ni Mbunge wa Makambako, Mhe. Deo Sanga, amesema katika mkoa huo ilani ya CCM inatekelezwa kwa kasi kubwa kwani mabilioni ya fedha yameelekezwa huko kuanzia barabara hiyo bilioni 11.3 imepelekwa, na barabara ya Kibena-Lupembe (km 42) kwa bilioni 75, Kitulo-Iniho (km 36. 3) kwa bilioni 82, Njombe-Moronga -Makete (km 117.5).
Akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Mhandisi Jephason Nko, amesema kuwa maendeleo ya mradi wa ujenzi wa sehemu ya barabara ya Itoni-Lusitu umefikia asilimia 21.6 na umeweza kutoa ajila kwa watanzania 380.
Ameongeza kuwa wameshalipa fidia kwa wananchi 190 waliopisha mradi huo kiasi cha shilingi bilioni 2.1 sawa na asilimia 57.24 kati ya wananchi 290 ambao barabara imewafuata.
Barabara ya Itoni - Lusitu ni sehemu ya utekelezaji wa barabara ya Itoni-Ludewa-Manda (km 211.4) ambayo inajengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Disemba 2024.