Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Bilioni 11 zakarabati Kiwanja cha Ndege cha Arusha


Serikali imewekeza jumla ya Shilingi Bilioni 11 kwa ajili ya kufanya maboresho ya miundombinu katika Kiwanja cha Ndege cha Arusha ili kuwezesha ndege kubwa na nyingi zaidi kutua kwenye kiwanja hicho na hivyo kuongeza pato la Taifa.

Akikagua maboresho yanayoendelea kwenye Kiwanja hicho kilichopo mkoani Arusha, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara (TANROADS), kusimamia kikamilifu maboresho hayo ili yaweze kukamilika kwa mujibu wa mkataba na kwa taratibu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Anga - ICAO.

“Kiwanja hiki ni kinaingizia Serikali fedha nyingi kutokana na upokeaji wake wa idadi kubwa ya watalii hivyo hakikisheni mnasimamia kikamilifu maboresho haya sambamba na kuboresha huduma kwa wateja wenu ili ndege nyingi zaidi ziendelee kutua katika Kiwanja hiki”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Ameongeza kuwa Kiwanja cha Ndege cha Arusha ni kati ya viwanja vitatu vya ndege nchini, vinavyopokea idadi kubwa ya ndege na abiria kwa siku, kikiongozwa na viwanja vya ndege vya Dar es Salaam na Mwanza.

Kwa upande wake, Meneja wa TAA mkoa wa Arusha, Mhandisi Elipigi Tesha, amemuambia Naibu Waziri Kasekenya kuwa hadi sasa maboresho yaliyokwishafanyika yamegharimu kiasi cha shilingi Bilioni Tano (5), ambapo kazi zilizofanyika ni uongezaji wa barabara za kuruka na kutua ndege mita 200 na kufika urefu wa mita 1,860 na kutawezesha ndege nyingi zaidi kutua kwenye kiwanja hicho.

Kazi nyingine ni ujenzi wa maegesho ya kisasa ya magari, pamoja na kufunga mfumo wa kisasa wa kukusanya mapato yaani Autopay System ambao umeongeza makusanyo ya kiwanja lakini pia mfumo huo umeongeza hali ya usalama katika Kiwanja cha Ndege cha Arusha.

Mhandisi Tesha ameongeza kuwa miradi iliyoko mbeleni itagharimu kiasi cha shilingi Bilioni Sita (6) ambapo zitajumuisha uboreshaji wa maeneo ya kuegeshea ndege pamoja na upanuzi wa jengo la abiria litakalowezesha kuchukua abiria 350 kwa wakati mmoja badala ya 190 kama ilivyo sasa.

Mhandisi Kasekenya amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili jijini Arusha, kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali inayosimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.