Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA KUMPIMA MENEJA MPYA TANROADS DAR KWA DARAJA LA JANGWANI


WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam Eng. John Mkumbo kuhakikisha Daraja la Jangwani linazibuliwa vizuri na maji yanapita kwa urahisi katika kipindi chote cha mvua za vuli.

Akizungumza alipokagua Daraja la Jangwani, jijini Dar es Salaam leo, Bashungwa amesema kazi ya kuzibua tope katika Daraja la Jangwani, ndio kitakuwa kipimo cha Eng. Mkumbo ambaye ameripoti katika nafasi hiyo hivi karibuni.

“Meneja TANROADS najua umeripoti haijapita hata mwezi kwenye mkoa huu, kama meneja wa mkoa, ili niweze kujiridhisha kwamba unatosha kipimo chako cha kwanza ni hapa kwenye kuzibua tope lililopo chini ya Daraja la Jangwani,” alisema Waziri Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema anataka kupata mrejesho wa kazi ya uzibuaji wa daraja hilo mara kwa mara ili kujiridhisha na utekelezwaji wa agizo lake.

Bashungwa amesema utekelezwaji wa agizo hilo ni mkakati wa muda mfupi wakati maandalizi ya ujenzi wa Daraja jipya la Jangwani lenye upana wa mita 43.2, urefu wa mita 390 na barabara unganishi zenye urefu wa mita 720 ukiendelea.
Daraja hilo jipya linatarajiwa kuanza ujenzi wake mwezi Februari mwakani ambalo linatarajiwa kuwa ufumbuzi wa changamoto ya kuziba mara kwa mara katika eneo hilo.

 

Kwa upande wake, Msimamizi wa Maandalizi ya Ujenzi wa Daraja hilo, Eng. Doroth Mtenga amesema Daraja hilo ambalo litakuwa na barabara za watembea kwa miguu, magari, bajaji na barabara ya mwendo kasi litaanzia eneo la Magomeni hadi eneo la Fire.