Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AZIKUTANISHA TEMESA NA AZAM MARINE UBORESHAJI HUDUMA ZA VIVUKO


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameukutanisha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Kampuni ya M/S Azam Marine kujadili namna ya kuendelea kushirikiana kwa pamoja kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni – Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimefanyika Mei 10, 2024 jijini Dar es Salaam kwa kuwakutanisha Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, timu ya watalaam kutoka TEMESA na uongozi wa Azam Marine ukiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Azam Marine, Abubakar Aziz.

Waziri Bashungwa ameitaka TEMESA kubadilisha mtazamo wao katika utoaji huduma ili waweze kujiendesha kibiashara kama Sekta Binafsi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za usafiri wa vivuko nchini.

“TEMESA nyie ni watoa huduma, hivyo lazima mbadili mitazamo yenu na kujiendesha kama Sekta Binafsi sambamba na kuweka mifumo madhubuti itayosaidia utoaji wa huduma zenu kuwa bora”, amesisitiza Bashungwa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko kutoka TEMESA, Eng. Sylvester Simfukwe ameeleza kuwa TEMESA ililazimika kutafuta njia mbadala ya kuhakikisha huduma inaendelea katika eneo la Magogoni – Kigamboni mara baada ya Kivuko cha MV. Kazi kupelekwa kufanyiwa ukarabati mkubwa na iliingia makubaliano na Kampuni ya Azam Marine ya kushirikiana kutoa huduma ya usafiri wa vivuko kulingana na mahitaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Azam Marine, Abubakar Aziz ameeleza kuwa Azam Marine kwa sasa wanakodisha Sea tax mbili kwa TEMESA katika kituo cha Magogoni – Kigamboni ambavyo vinatoa huduma masaa 8 kwa siku na kusafirisha abiria 3,000 kwa saa na abiria 24,000 ndani ya siku moja.