Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AWATAKA WATUMISHI UJENZI KUSHIRIKIANA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewahimiza Watumishi wa Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Taasisi zake ili kuhakikisha mipango na mikakati ya Serikali inayoandaliwa inatekelezwa kwa wakati, tija na ufanisi.

Akizungumza katika kikao kazi na watumishi wa Wizara hiyo jijini Dodoma Bashungwa amesema kufanya kazi kwa kushirikiana kwa uwazi na kubadilishana uzoefu kutaiwezesha Wizara hiyo kuwa na mipango shirikishi inayotekelezeka na kupimika na hivyo kupunguza changamoto ya Wizara kuwa na mipango inayotofautiana na Taasisi zake katika usanifu na utekelezaji.

“Fanyeni kazi kama timu moja ili kupata uzoefu mpana miongoni mwenu na ongezeni ubunifu katika kubuni miradi ili iwe ya kisasa na itakayodumu kwa muda mrefu”, amesema Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa amezungumzia umuhimu wa watumishi kujibu hoja na changamoto za wananchi kwa wakati na kuhakikisha taarifa za upotoshaji zinajibiwa kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kuwa na taarifa sahihi kuhusu miradi inayoendelea katika maeneo yao.

Aidha, amewataka watumishi wa Wizara kufanya kazi kwa uwazi, upendo na ushirikiano miongoni mwao ili kuleta motisha kwa watumishi na hivyo kuwawezesha kuwa wabunifu.

“Watumishi wote wa Wizara ya Ujenzi fanyeni kazi kwa ubunifu kuweni huru kufanyakazi na kuleta maoni yenu kwa viongozi ili matarajio ya Serikali yafikiwe kwa wakati”, amesisitiza Bashungwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya amezungumzia umuhimu wa viongozi wa Taasisi, Idara na Vitengo kufanya uamuzi sahihi ili kuondoa malalamiko kwa watumishi na wananchi na hivyo kuleta taswira chanya kwa wizara kwa ujumla.

“Kila kiongozi awe na maono katika sehemu anayoiongoza na maono hayo yawe shirikishi kwa wataalam wake ili mikakati ya kuyatekeleza iwe rahisi na yenye tija”, amesisitiza, Kasekenya.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Bw. Ludovick Nduhiye amemhakikishia Waziri Bashungwa kuwa Wizara hiyo itaendelea kuwa shirikishi kwa watumishi wake na kuwapa motisha kila inapobidi ili malengo tarajiwa ya Serikali yafikiwe.

Kikao hicho chenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja na kubadilishana uzoefu kimehudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Naibu Waziri wa Ujenzi, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi na Watumishi wote wa Wizara hiyo.