Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AWATAKA MAMENEJA TANROADS NA TARURA KUSHIRIKIANA KUKABILI ATHARI ZA MVUA ZA VULI


WAZIRI wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na Mameneja wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kushirikiana kikamilifu katika kipindi hiki cha mvua za vuli ili kuhakikisha barabara zote nchini haziathiriki na mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote.

Akizungumza alipokagua Daraja la Jangwani, Barabara ya Mwendokasi, Barabara ya Njia nane Kimara-Kibaha, Kibamba shule –Mpiji Magoe KM 9.2 na Barabara ya Kimara-Bonyokwa-Kinyerezi KM 7, jijini Dar es Salaam.

Bashungwa amewataka watendaji wote wa Wakala hizo kwenda maeneo ya kazi ili kuhakikisha mifereji ya maji inazibuliwa na athari zinazojitokeza wakati wa mvua zinadhibitiwa kwa wakati.


“Sisi Mawaziri tunashirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za miundombinu hivyo naagiza kuanzia sasa Watendaji Wakuu wa TANROADS na TARURA, Mameneja na wafanyakazi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwaondolea kero wananchi na hivyo kusafiri kwa uhakika,” amesema Waziri Bashungwa.

Amewataka wananchi kuacha kutupa taka hovyo katika mitaro ya barabara na mabonde ya maji na kuacha shughuli za uchimbaji mchanga pembezoni mwa madaraja hali inayosababisha mmomonyoko wa udongo na kusababisha uharibifu wa barabara na madaraja.
 Amewaonya wananchi na taasisi mbalimbali kuacha kutumia hifadhi za barabara kufanya biashara kwani kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na usalama wa watu na mali zao na kuwataka Mameneja wote wa TANROADS nchini kuhakikisha hifadhi za barabara zinalindwa.

 

Kwa upande wake Waziri wa TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru Waziri wa Ujenzi kwa ushirikiano anaompa na kumhakikishia ushirikiano huo utaendelezwa hususan katika ujenzi wa Daraja la Jangwani na Bonde la Msimbazi ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi hakikisheni usafi wa mazingira unapewa kipaumbele katika maeneo yenu ili kuruhusu maji ya mvua yaweze kupita kwa urahisi na hivyo kutoleta athari kwa miundombinu,” amesisitiza Waziri Mchengerwa.
 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila amewataka wananchi kutoa taarifa kwa haraka pindi wanapobaini athari za barabara na madaraja ili kuepuka madhara zaidi

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya barabara na madaraja jijini Dar es salaam kuona athari za mvua na kutoa maelekezo ya hatua za haraka kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.