Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA ATOA SIKU 4 KIVUKO CHA MV. MARA KUKAMILISHWA NA KUANZA KUTOA HUDUMA.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameitaka kampuni ya Songoro Marine kuhakikisha inakamilisha ukarabati wa kivuko cha MV. Mara kinachofanya safari zake kati ya Iramba wilaya ya Bunda na Majita wilaya ya Musoma Vijijini ndani ya siku nne na kuanza kutoa huduma ifikapo Oktoba 15, 2023.
 

Amesema hayo leo tarehe 11 Oktoba 2023 jijini Mwanza wakati alipotembelea karakana ya kutengeneza na kukarabati vivuko ya Songoro Marine Ltd, kujionea vivuko tisa vya Serikali vinavyojengwa na kukarabatiwa na karakana hiyo.
 

Waziri bashungwa amesema alipokuwa kwenye ziara Musoma Vijiji alipokea ombi la wananchi kutaka kivuko hicho kirejeshwe kwani kimechukua muda mrefu tokea kipelekwe kufanyiwa ukarabati.

“Niwaletee habari njema wananchi wa Musoma Vijijni na visiwa ambavyo vilikuwa vinapata huduma ya kivuko cha Mv Mara kuwa ukarabati wa kivuko hicho umefikia asilimia 99 na kitakuwa kimekamilika kufikia Oktoba 15, 2023 ili kirejeshwe na kuanza kutoa huduma ya usafiri” amesema Bashungwa.

Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Shilingi milioni 321.9 kukarabati kivuko hicho.

Aidha, Bashungwa amezitaka Taasisi na Mamlaka zote zinazohusika na ukaguzi na utoaji wa vibali baada ya ukarabati kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote ndani ya siku nne ili kuwezesha kivuko hicho kurejeshwa Mkoani Mara kuanza kutoa huduma.

Kadhalika, Bashungwa amevitaja vivuko vingine vinavyojengwa na kukarabatiwa katika karakana hiyo ni Rugezi Kisorya kimefikia 70%, Ijinga Kahangala – 67%, Bwiro Bukundo – 70%, Nyakalilo Kome – 55.5, Buyagu Mbalika – 30%, Mv. Nyerere – 79.5%, Mv. Kilombero – 84% na Mv. Ruhuhu – 90%.

Naye, Mkurugenzi wa Songoro Marine Ltd, Major Songoro ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaamini na kupewa kazi za kujenga na kukarabati vivuko vya Serikali na ameahidi kufanya kazi kwa weledi na kwa mujibu wa mikataba.