Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA ATOA POLE, AAGIZA MAWASILIANO YA BARABARA DAR KUREJESHWA HARAKA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Eng. Godfrey Kasekenya kufika katika maeneo yaliyoathiriwa  na mvua  mkoani Dar es Salaam na kuungana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS),  Eng. Mohamed Besta, pamoja  na timu ya wataalam kuhakikisha wanachukua hatua za haraka kwa kurejesha mawasiliano ya barabara na madaraja yaliathiriwa ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao.

Ameeleza hayo wakati akitoa pole kwa wananchi wa mkoa wa Dar es salaam  kupitia Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila kufuatia mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia leo Tarehe 20 Januari, 2024 na kuharibu miundombinu mkoani humo.

“Hivi ninavyozungumza Naibu Waziri yupo njiani anaelekea Dar es Salaam kuungana na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, pamoja na timu ya wataalam kufika mara moja maeneo ambayo mawasiliano ya barabara yamekatika ili tuanze kuchukua hatua za haraka kuahkikisha mawasiliano yanarudi”, amesema  Bashungwa

Aidha, Bashungwa amewaagiza TANROADS kuendelea kushirikiana na TARURA kuhakiksha wanarudisha miundombinu yote inayoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.