Habari
BASHUNGWA ATOA MWEZI MMOJA KWA WAHANDISI WOTE NCHINI KUWA NA LESENI.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka Wahandisi na Washauri elekezi wote nchini kuhakikisha wanakuwa na leseni zinazowapa uhalali wa kufanya kazi za kihandisi nchini ifikapo tarehe 31 Machi 2024.
Amesema hayo Februari 26, 2024 Dar es salaam katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 21 ya Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahandisi Wahitimu (SEAP) na uzinduzi wa ufadhili kwa wahandisi wa kike, unaofadhiliwa na Serikali ya Norway.
“Wahandisi wote, wataalamu na washauri hakikisheni mnakuwa na leseni za uhandisi. Leseni hizi zinawapa uhalali wa kufanya kazi za kihandisi nchini, Kila mhandisi mtaalamu au mshauri lazima awe na leseni hai ifikapo 31 Machi 2024”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa kuanzisha utaratibu wa kuwaapisha wahandisi wataalamu wote kwani taaluma hiyo ni nyeti sana kwa uchumi wa nchi, usalama wa mazingira na maisha ya watu na mali zao.
Amewaagiza Wahandisi wote kuzingatia mafunzo ya kujiendeleza (Continue Professional Development (CPD), ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia zinazobadilika kila wakati na haraka sana kila siku.
Aidha, amesema Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahandisi Wahitimu (SEAP) umekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza ujuzi wa wahandisi wahitimu nchini kwa kuwawezesha kupata uzoefu wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira.
“Takwimu zinaonyesha tangu kuanzishwa kwa SEAP mwaka 2003, imewapa mafunzo kwa vitendo wahandisi wahitimu zaidi ya 12,000. Kati yao 3,018 ni wanawake, hii ni hatua kubwa katika kuelekea usawa wa kijinsia katika sekta ya uhandisi” amesema Bashungwa.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha mpango wa SEAP kwa kuhakikisha upatikanaji wa nafasi za mafunzo kwa wahandisi wahitimu zinakuwa za kutosha pamoja kuboresha mazingira ya mafunzo.
Kadhalika, Bashungwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Chini ya Uongozi Dr. Hussein Mwinyi, zimedhamiria kuimarisha taaluma ya uhandishi kupitia programu mbalimbali.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bi Khadija Khamis Rajab amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaitendea haki fursa ya Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahandisi Wahitimu (SEAP) kwa wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na Mafunzo hayo.
Nae, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng. Bernard Kavishe amesema Mpango wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahandisi Wahitimu (SEAP) utazalisha wataalam wengi wazawa na kuwapatia ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.