Habari
BASHUNGWA ATOA MWEZI MMOJA KUKAMILISHA USANIFU DARAJA LA MUNGURI – KONDOA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuhakikisha anakamilisha Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Daraja la Munguri lililopo katika Mto Bubu ulilopo wilayani Kondoa mkoani Dodoma.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 4 Disemba 2023, alipokagua eneo hilo la Daraja linalokatisha barabara ya Kondoa - Mtiriangwi/Gisanbang inayounganisha Mkoa wa Dodoma, Singida na Manyara, Wilayani Kondoa.
"Nitumie nafasi hii kumuelekeza Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dodoma, Usanifu wa Daraja hili ufanyike mapema, na inapofika wiki ya Kwanza ya Januari 2024 nipate Ripoti ya kukamilika Kwa Usanifu wa Daraja hili, ili kupata gharama za ujenzi ili ziwekwe kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24"Amesema Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa amesema Daraja hilo ni muhimu sana kujengwa kwa kuwa ni daraja kubwa la kitaifa linalounganisha mikoa mitatu, na Mvua zinaponyesha Wananchi wanakosa Mawasiliano kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Vilevile, Waziri Bashungwa amemshukuru Mheshimiwa Rais Wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu Nchini, Hasa kwenye Mkoa wa Dodoma ambapo kuna miradi mingi ambayo inaendelea kutekekelezwa kwa maelekezo yake.
"Kwa Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ameniagiza nifike hapa na niangalie vipaumbele na kufanya upembuzi yakinifu Kwa kujenga Daraja la kudumu katika Wilaya ya Kondoa"amesema Waziri Bashungwa
Kwa Upande wake, Mbunge wa Kondoa Vijijini ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji ameiomba Serikali kupitia Wizara ya ujenzi kuweza kujengewa Daraja la Mto Bubu kwani limekuwa kikwazo wakati wa Mvua.
"Daraja hii ni muhimu sana Kwa wakazi wa Kondoa, Manyara na Singida Kwa ujumla Kwa sababu ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na pia ni Daraja tegemezi Wilayani hapa kwa usafirina usafirishaji", amesema Dkt kijaji.
Awali, akitoa taarifa kuhusu daraja hilo Meneja wa Mkoa wa Dodoma wa TANROADS, Eng. Leonard Chimagu amesema kuwa Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo unatekekelezwa na Serikali kwa kutumia fedha za ndani na Mhandisi Mshauri Crown- Tech Consult Ltd. kwa gharama ya milioni 480.8 na fedha ya utekelezaji wa kazi hiyo umetengwa katika mwaka huu wa fedha.
Kukamilika Kwa Daraja hili kutaleta faida mbalimbali za kiuchumi katika Mkoa wa Dodoma, Singida na Manyara.