Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA ATOA MIEZI MIWILI KWA MKANDARASI KUKAMILISHA DARAJA LA MTO RUAHA MKUU – KILOMBERO


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametoa miezi miwili kwa Mkandarasi wa Kampuni ya M/s Reynolds Construction v kukamilisha ujenzi wa  Barabara ya Mikumi-Kidatu-Ifakara, sehemu ya Kidatu-Ifakara (Km 66.9) kwa kiwango cha lami pamoja na Ujenzi wa Daraja  la Mto Ruaha Mkuu.

Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo leo tarehe 23 Februari 2024, wilayani Kilombero mkoani Morogoro mara baada ya kukagua Barabara hiyo na Daraja la Mto Ruaha Mkuu na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi ambapo Mkandarasi yupo nje ya muda wa mkataba wa kukamilisha mradi huo.

“Sijaridhishwa na kasi ya mkandarasi, hivyo nimempa miezi miwili awe amekamilisha hii barabara,  asipofanya hivyo akija kuomba kazi yoyote ndani ya nchi hii hatuwezi kumpatia”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa Mkandarasi ameshalipwa Fedha zote za kutekeleza mradi huo kwa wakati na Daraja hilo linajengwa kwa viwango imara Sambamba na Ujenzi wa Barabara zake.

Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka barabara hiyo iwe barabara ya kitaifa kwani inaunganisha Mkoa wa Tanga-Morogoro-Njombe pamoja na nyanda za juu kusini hadi kufika bandari ya Mtwara.

“Kuanzia bandari ya Tanga-Handeni kuja Turiani-Kilosa-Mikumi kupita Kidatu-Kilombero kwenda ifakara -Mlimba hadi lupembe mkoani Njombe hadi Kibena inaunganishwa kwa kiwango cha lami” amesema Bashungwa

Akitoa Taarifa ya Mradi, Meneja wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema ujenzi wa barabara hii unafadhiliwa na mfuko wa maendeleo wa Nchi za ulaya, ukishirikiana na shirika la Msaada la Uingereza ( UKAID) pamoja na Shirika la Kimarekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

Vilevile, ameongeza  kuwa Ujenzi wa barabara hiyo na Daraja la Mto Ruaha Mkuu ni sehemu ya mkakati wa Taifa  kusaidia wakulima wadogo kupitia program ya Uendelezaji kilimo katika Ukanda wa kusini mwa Tanzania-SAGCOT, walioko katika Bonde la Mto Kilombero ili kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao kipindi chote cha mwaka.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilombero, Abubakar Asenga, amesema daraja hilo ni sehemu ya Barabara ya Kidatu -Ifakara na ni daraja ambalo linasubiliwa sana na Wananchi hao kwani kukamilika kwake kutafungua Fursa kwa wakazi wa kilombero na Mkoa kwa ujumla.

Naye, Mbunge wa Mikumi Denis Londo, ameishukuru Serikali ya Awamu ta sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa iliyofanyika ya utekelezaji katika Mkoa wa Morogoro.