Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AMTAKA MKANDARASI DARAJA LA ITEMBE KULIKAMILISHA KABLA YA EL-NINO.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua ujenzi wa Daraja la Itembe (mita 150) linalounganisha mkoa wa Singida na Simiyu na kumtaka mkandarasi wa kampuni ya Rocktronic kukamilisha ujenzi wake kabla ya mvua za El - Nino kuanza.

Ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 65 na unatekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 6.8.

Agizo hilo amelitoa mkoani Simiyu wakati alipokua ziarani kukagua miradi ya barabara, madaraja inayoendelea kutekelezwa mkoani humo ambapo pamoja na mambo mengine ameridhishwa na ubora wa mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi wa ndani.

"Nafurahi kukagua mradi huu na kukuta mkandarasi mzawa ndio wanaofanya kazi hii kwa kiwango cha kuridhisha hilo lazima niwapongeze TANROADS kwa usimamizi mzuri", amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameagiza mkandarasi huyo kulipwa mapema malipo yake anayodai ili kazi isisimame na wafanye kazi usiku na mchana.


"Mheshimiwa Rais ameshatoa fedha kwa ajili ya madeni ya makandarasi wa ndani hivyo basi mkandarasi huyu alipwe mapema iwezekanvyo ili mvua za El-Nino zisilete madhara kwa wannachi wa mikoa hii miwili ambao wamekuwa wakikosa mawasiliano ya barabara vipindi vya mvua", amesisitiza Bashungwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luaga Mpina amemuomba Waziri huyo kujenga madaraja mengine ya Chobe, Nkoma, Liusaambayo nayo imekuwa kikwazo kikubwa katika barabara ya Meatu- Sibiti mkoani Simiyu.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa madaraja hayo kutarahisisha ujenzi wa barabara hiyo pindi itakapoanza kutekelezwa kwa wakati.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara(TANROADS) mkoa wa Simiyu, Mha. John Mkumbo ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja hilo utakuwa na nguzo saba na eneo la watembea kwa miguu kila upande.

Ujenzi wa Daraja la Itembe ulitokana na mto Itembe ambapo kipindi cha mvua hujaa maji na kuleta maafa na wananchi kushindwa kuvuka kuelekea upande ya pili na kulazimika kusubiri kwa kipindi kirefu  ili waweze kuvuka.