Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AMKABIDHI MKANDARASI HENAN BARABARA KM 77.6 SINGIDA


Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kumsimamia kikamilifu Mkandarasi Henan Highway Engineering Group anaejenga barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga KM 77.6 ili ikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Amesema hayo Misigiri Iramba mkoani Singida katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway ujenzi wa barabara hiyo.

" TANROADS jipangeni vizuri ujenzi ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora", amesema Mhe. Bashungwa.

Waziri huyo wa ujenzi amewataka wananchi watakaopata ajira katika mradi huo kuwa waaminifu, wabunifu na walinzi wa vifaa vya mkandarasi ili kutouchelewesha mradi huo na kujiongezea ujuzi ili utakapokamilika wawe wamenufaika maradufu.

" Tunataka mradi huu uendane na thamani ya fedha na barabara hii kwakuwa itachochea uchumi ni vema wananchi mkatumia fursa za biashara na uzalishaji wa mazao zitakazosababishwa na uwepo wa barabara hii kukuza uchumi", amesema Waziri Bashungwa.

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema barabara hiyo inayounganisha wilaya za Singida, Ikungi na Iramba itahuisha uchumi kwa wakazi wa mkoa wa Singida kwa kuwa inapita kwenye maeneo ya kilimo na madini.

Amesema zaidi ya shilingi bilioni 88.5 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo.

Nae Mbunge wa Iramba ambaye pia ni Waziri wa Fedha Mhe. Mwigulu Nchemba ameishukuru Serikali kwa namna inavyozifungua barabara za mkoa wa Singida na kuwataka wakazi wa mkoa huo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo.

Mkuu wa mkoa wa Singida Bw, Peter Serukamba amamhakikishia Waziri wa Ujenzi kuwa vifaa vya mkandarasi vitalindwa na atapata ushirikiano ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

“Tunaishukuru serikali kwa kuwa barabara zetu kubwa mkoani singida zinajengwa kwa kiwango cha lami na hivyo kuufanya mkoa wetu kufikika kirahisi toka pande zote za nchi nasi tumejipanga kuongeza uzalishaji wa vitunguu, alizeti,ufuta,mahindi na ufugaji wa kuku”, amebainisha mkuu wa mkoa Serukamba.

Hafla ya kukabidhi barabara hiyo kwa mkandarasi pia imehudhuriwa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Mhe. Kitila Mkumbo ambaye amesema moja ya mipango ya Serikali ni kuhakikisha mabonde ya kilimo likiwemo la iramba yanawekewa miundombinu bora ya umwagiliaji ili yatumike wakati wote wa mwaka.

Kukabidhi barabara hiyo kwa mkandarasi kunafuatiwa kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wake Agosti 7 mwaka huu.