Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AAGIZA TIMU YA WATAALAM KUREJESHA MIUNDOMBINU LINDI


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Eng. Aisha Amour kupeleka timu ya wataalam mkoani Lindi itakayohakikisha inasimamia urejeshwaji wa miundombinu yote ya barabara na madaraja iliyokatika kutokana na kujaa maji hivyo kusababisha huduma za usafiri na usafirishaji kusimama katika Wilaya za Liwale, Nachingwea, Ruangwa na Masasi.

Bashungwa ametoa agizo hilo Mkoani Lindi akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi kukagua maeneo yote yaliyojaa maji na kusababisha barabara na madaraja kukatika katika Wilaya hizo na kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Wakala wa Barabara (TANROADS), wa Mkoa huo.

“Tumekagua barabara na madaraja kutoka Liwale, Nachingwea, Ruangwa na Masasi kazi inayoendelea kufanywa na Makandarasi hairidhishi, Hii kazi ni ngumu na bado ni Kubwa, Sasa nimuelekeze Katibu Mkuu wa Wizara kuleta timu ya watalaam ipige kambi hapa na ninataka ndani ya muda mfupi barabara zipitike”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ametoa siku saba kwa timu hiyo ya wataalam kuwasimamia Wakandarasi waliopewa kazi ya urejeshaji wa barabara na madaraja na kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku kama ilivyokuwa awali.

Aidha, amemuagiza Mkandarasi anayejenga barabara ya Nanganga – Ruangwa   kwa kiwango cha lami kuhakikisha maeneo yote yaliyojaa maji katika barabara hiyo yanapatiwa ufumbuzi kwa kuyachepusha kwenye madaraja ambayo tayari yamekwishamilika kujengwa na kuendelea na ujenzi wa madaraja mengine mapema iwezekanavyo.

“Hatuwezi kuacha wananchi wanahatarisha maisha yao katika hali hii, kuanzia sasa hivi mitambo ije, kazi ya kuchepusha maji katika eneo hili kuelekea kwenye daraja ifanyike na ujenzi wa daraja katika Mto Lukuledi ianze kufanyika usiku na mchana”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itafanya kila jitihada ya kurudisha huduma za Mawasiliano kwenye maeneo yote yenye changamoto ya kujaa maji na kukatika kwa barabara na madaraja.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amesema kuwa Serikali imesikia kilio cha wana Lindi na ndiyo maana imetuma Viongozi kuja na kukagua maeneo yote yenye changamoto na kutoa ufumbuzi.