Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AAGIZA MAMENEJA WA TANROADS KUKARABATI MIFEREJI YA BARABARA.


Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amewaagiza Mameneja wa Mikoa wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mikoa yote nchini kukarabati mifereji iliyo pembezoni mwa barabara kuu ili kuzuia athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua ikiwemo kuharibika kwa barabara.

Bashungwa ametoa agizo hilo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta aliyeuliza kuhusu ni lini Wizara Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi itasafisha mifereji iliyozibwa wakati wa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo.

"Nitumie nafasi hii niwaelekeze Mameneja wa TANROADS mikoa yote nchini kufika kwenye maeneo ambayo yana changamoto kama wabunge walivyosema na kuona namna ambavyo tunaweza kukakabiliana na jambo hili kwa dharura na haraka", amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema Serikali inajipanga kutafuta namna ya kuwaondolea adha ya mafuriko wananchi katika barabara ya Mwenge - Bagamoyo.

Naye, Mbunge wa Kawe Askofu Josephat Gwajima alitaka kujua ni lini ujenzi wa barabara ya Mabasi yaendayo haraka inayoanzia Mwenge - Tegeta - Basihaya itaanza kujengwa.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema hatua iliyopo kwa sasa ni hatua ya awali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo na tayaru mkandarasi yupo eneo la ujenzi.

"Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge hatua iliyopo sasa hivi ni hatua za awali (mobilization) kwa ajili ya kuanza kuijenga barabara hiyo na wakandarasi wapo wanafanya maandalizi ya awali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo", amesema Eng. Kasekenya.