Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA SONGEA – NJOMBE – MAKAMBAKO KUJENGWA UPYA: WAZIRI BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inatarajia kuanza kujenga upya barabara ya Songea – Njombe - Makambako kwa kiwango cha lami kutokana na barabara hiyo kuwa nyembamba na muda wake kuisha.

Bashungwa amesema hayo Wilayani Ludewa, mkoani Njombe wakati akizungumza na wananchi wa Mlangali katika mkutano wa hadhara ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kufungua mikoa na nchi jirani kwa barabara za lami.

Bashungwa amesema hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu Serikali itakuwa imempata Mkandarasi atakayenga upya barabara hiyo ikiwa ni dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

“Ukitoka bandari ya Mtwara unakuja kwa lami hadi Songea, na kutoka Songea kuja Njombe mjini kwenda makambako, lami ilijengwa miaka ya 80 imechoka, tayari Mheshimiwa Rais ametupatia fedha na kufika mwezi wa tatu au wa nne tutakuwa tumepata mkandarasi anakuja kuijenga upya”, amesema Bashungwa.

Bashungwa amewataka wananchi kuendelea kuheshimu Sheria na kutofanya shughuli katika maeneo ya hifadhi ya barabara ili kuondokana na usumbufu pale Serikali inapotumia Sheria zilizowekwa kuwaondoa katika maeneo ili kujenga miundombinu ya barabara.

Aidha, Bashungwa amesema Serikali itatoa shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya kuunganisha barabara inayotokea Wilaya ya Busokelo Mkoani Mbeya hadi Wilaya ya Makete mkoani Njombe kwa kiwango cha changarawe.

Ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais ameagiza kupelekwa Bilioni 1 kwa ajili ya kufanyia maboresho barabara ya Ikonda – Lupila – Mlangali ambayo imekuwa na changamoto hasa katika kipindi cha mvua.

Naye, Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga ameiomba Serikali kujenga barabara ya kilometa moja inayoelekea katika kituo cha Afya ambacho ndicho kimekuwa kikitoa huduma kubwa kwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Victoria Mwanziva, ameeleza kuwa wilaya hiyo ni wilaya ya kimkakati hivyo inahitaji miundombinu bora kwa ajili ya kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao, asali na bidhaa ndani na nje ya nchi.