Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA RAMADHANI – IYAYI KM 74 (WANGING’OMBE) KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema kuwa Serikali inakwenda kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ramadhani – Iyayi yenye urefu wa kilometa 74 ambayo imekuwa ni kilio kikubwa cha wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe, mkoani Njombe.

Hayo ameyasema mkoani humo katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Luduga katika Wilaya ya Wanging’ombe ambapo pamoja na mambo mengine amekagua barabara hiyo ambayo imewekwa lami baadhi ya sehemu na kubakia kilometa 53 ambayo inaenda kujengwa kwa kiwango cha lami.

“Barabara hii ni muhimu kwa ukanda wa Nyanda za Juu kusini na tayari Mheshimiwa Rais amekwishatoa maelekezo ya kuunganisha mikoa yote katika ukanda huu kwa barabara za lami kutoka Ruvuma, Njombe, Iringa Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi kwani ndio mikoa inayotegemewa sana kwa kilimo na kwa kuchapa kazi”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa barabara hiyo kwa uchumi wa nchi yetu Wizara ya Ujenzi inaenda kutenga bajeti katika Mwaka wa fedha ujao 2024/2025 kwa kuijenga kilometa 10 ili kuikamilisha kabisa barabara yote.

“Barabara hii imekuwa ikijengwa kilometa moja moja kila Mwaka sasa Mheshimiwa Rais amesema kwenye bajeti moja tuwe tunajenga kilometa 10 kwa Mwaka kwa kiwango cha lami ili kumaliza miradi ya barabara kwa wakati”, amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais ameridhia ukarabati wa barabara ya Songea - Makambako - Njombe kwa kiwango cha lami ambayo ilijengwa miaka ya nyuma na tayari imekwishakaa.

Aidha, Amesema Mheshimiwa Rais amekwishatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 82 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Isyonje – Kitondo – Makete sehemu ya Kituko – Inilo (km 36.3) kwa kiwango cha lami pamoja na mzani wa kisasa utaoruhusu magari kupima magari yakiwa kwenye mwendo.

“Mzani huo utakuwa wa kisasa ambapo magari yakipita kutakuwa na taa zitakazonesha gari ikiwa imezidisha uzito kuingia ndani ikaguliwe na zile ambazo hazitazidisha uzito zitaruhusiwa kuendelea na safari”, amesema Bashungwa.

Ameeleza kuwa mzani huo unatakiwa ukidhi magari makubwa yatakayopitisha bidhaa na mazao kutokana na ukarabati mkubwa utakaofanyika katika barabara ya Songea - Makambako - Njombe na kuunganisha mikoa yote ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Bi. Veronica Sanga, amesema kukamilika kwa barabara hii kutafungua fursa kwa wakazi wa wanging’ombe  na Mkoa kwa ujumla kwani ndipo kunapozalishwa zao la parachichi na viazi kwa wingi.
 

Waziri Bashungwa yupo mkoani Njombe kwa ziara ya siku tatu ambapo atakagua  miundombinu ya barabara iliyokamilika na ile inayoendelea kutekelezwa.