Habari
BARABARA YA MASASI - MTWARA KUKARABATIWA UPYA

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema ukarabati wa Barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi yenye urefu wa kilometa 201 unatekelezwa na Serikali kwa fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia, ili kuharakisha utekelezaji wa kazi, mradi umegawanywa katika sehemu mbili ambapo mkataba kwa sehemu ya kwanza ya kutoka Mtwara – Mingoyo (km 82.27) na upanuzi wa Barabara kutoka njia mbili hadi njia nne katika Mji wa Mtwara (km 2.82) umesainiwa na sasa Mkandarasi yupo kwenye hatua za maandalizi ya kuanza ujenzi.
Pia Sehemu ya pili ya Mingoyo – Nanganga – Masasi (km 108.24) ipo kwenye hatua za mwisho za manunuzi ya kumpata mkandarasi na mkataba unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Februari, 2025.
Hayo yameelezwa Februari 3,2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Masasi Mjini Geoffrey Mwambe aliyeuliza ni lini Serikali itaanza kujenga upya Barabara ya Masasi, Mingoyo hadi Mtwara.
“Kwa sababu ya ukubwa wa mradi, mimi pamoja na Wizara tunamuhakikishia Mbunge kwamba tupo tayari kwenda wakati barabara hiyo itakapoanza kujengwa", amesema Eng. Kasekenya.