Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA KIMARA –KIBAHA NJIA NANE KUKAMILIKA OKTOBA


Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi anayejenga Barabara ya Kimara – Kibaha (Km 19.2), pamoja na Barabara za maingilio katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Mbezi-Magufuli kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kukagua barabara hiyo leo jijini Dar es Salaam, Eng. Kasekenya amesema Serikali imeridhishwa na uboreshaji wa barabara za maingilio na madaraja katika eneo la mbezi hivyo kumtaka mkandarasi kumaliza kazi hiyo haraka iwezekanavyo na kwa ubora.

Amebainisha kuwa katika mkakati wa kupunguza msongamano jijini Dar es salaam tayari maandalizi ya kujenga kwa njia nane sehemu ya Kimara hadi Ubungo yameanza ili kuhakikisha hakuna msongamano wa magari kati ya  Ubungo-Kibaha.

“..Asilimia themanini na nane iliyofikia inatosha kukamilisha kazi zilizobaki katika kipindi cha miezi miwili ijayo, hivyo TANROADS na Mkandarasi ESTIM hakikisheni kazi hiyo inakamilika kwa ubora,” alisisitiza Eng. Kasekenya.

Aidha amewaonya wezi wa miundombinu ya taa za barabara kuacha kufanya hivyo mara moja kwani usalama wa barabara ni pamoja na uwepo wa taa hizo, na kusisitiza umuhimu wa wananchi kutumia madaraja ya juu na kuvuka katika maeneo yaliyotengwa ili kupunguza ajali.

Naye Mhandisi Mkazi anayesimamia ujenzi wa Barabara hiyo, Injinia Mwanaisha Rajabu amemhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa atahakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa ifikapo Oktoba.