Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA SALAMA KIPAUMBELE TANZANIA


SERIKALI imewataka wadau wote wa miundombinu ya barabara kushirikiana ili kuhakikisha barabara zote nchini zinakuwa salama kwa kwa watumiaji wote na wakati wote.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Saad Mtambule alipokuwa akimwakilisha Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa katika hafla ya kufunga mradi wa majaribio wa mpango wa hatua kumi (Ten step plan), wa miundombinu ya barabara salama nchini Tanzania.

Mpango huo uliotekelezwa kwa miezi 30 kwa kudhaminiwa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Usalama Barabarani na Benki ya Dunia unalenga kuzipa hadhi barabara nchini kutoka nyota moja hadi tano kutokana na uwezo wake wa kutosababisha ajali na hivyo kulinda maisha na mali kwa watumiaji wa barabara.

“…Serikali inathamini jitihada za wadau wote wa barabara ikiwemo Benki ya Dunia, Shirikisho la Barabara la Kimataifa (IRF), Mpango wa Kimataifa wa Tathmini ya Barabara (iRAP) na Chama cha Wadau wa Barabara nchini Tanzania (TARA) kwa kuiwezesha Tanzania kuwa nchini ya kwanza duniani kutekeleza mradi huo wa majaribio ya barabara salama ,” amesema DC Mtambule.

Naye Mkurugenzi wa Barabara wa wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Eng. Alois Matei amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wake imejipanga kuhakikisha barabara zinazojengwa zinakuwa na alama zote za usalama barabarani na zinatenganisha maeneo ya watembea kwa miguu, waendesha baiskeli na magari  ili kupunguza ajali.

Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha bajeti zake kila mwaka  ili katika ujenzi wa barabara mpya usanifu wake uzingatie viwango vyote vya usalama barabarani na kuondoa vikwazo kwenye maeneo yanayosababisha ajali mara kwa mara.

Zaidi ya watu milioni moja na laki nne wanahofiwa kuwa hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na ajali za barabarani zinazosababishwa pamoja na mambo mengine uwepo wa barabara zisizo salama.