Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA NJIA NNE KUJENGWA JIJINI MBEYA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Igawa-Uyole-Songwe-Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa njia nne (4) kutawaondolea wananchi kero ya msongamano na ajali na hivyo kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa wakati.

Akizungumza jijini Mbeya wakati wa utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya Msalaga hadi Airport yenye urefu wa Kilomita (32) Prof. Mbarawa amewataka wakazi wa mkoa wa mbeya na Songwe kuchangamkia fursa za uzalishaji ili kunufaika uwepo wa barabara hiyo.

“Bidhaa za Nchi za Malawi, Zambia na Kongo zinazokwenda na zinazotoka bandari ya Dar es Salaam zitafika kwa urahisi itakapokamilika barabara hii hivyo ni wakati kwa wakazi wa Nyanda za juu Kusini kutumia fursa ya uwepo wa barabara hiyo itakapokamilika’ amesisitiza Waziri Prof Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa katika ujenzi wa barabara  hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili kuchochea uchumi wa wananchi wa mikoa ya Mbeya na Songwe.

“Nia ya Serikali ni kuhakikisha inaboresha miundombinu ili wananchi watumie fursa hizo kukuza uchumi binafsi na Taifa kwa ujumla’ amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Kwa upande Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dkt Tulia Ackson ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu nchini hususani mkoani Mbeya hali itakayochochea kupanda kwa uchumi wa Mkoa na Taifa kwa ujumla

‘Barabara hiyo inayounganisha Tanzania na Nchi za Malawi na Kongo ikikamilika itakuza biashara katika jiji la Mbeya’amesema Spika Tulia.  

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa wakala huo umejipanga vizuri kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Mradi huo utakaojengwa na Kampuni ya China Henan International Coorporation Group Co. ltd (CHICO) unatarajiwa kutumia miezi 24 na utagharimu  zaidi ya shilingi bilioni 138 utakapokamilika.

Barabara ya Igawa-Uyole-Songwe-Tunduma ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM na barabara kuu ya nne inayotoka Cape Town Afrika ya Kusini hadi Cairo nchini Misri.