Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

ZAIDI YA KILOMETA 200 ZIMETENGWA KWA  WAKANDARASI WA NDANI


Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema imetenga jumla ya miradi minne ya ujenzi wa barabara zenye jumla ya urefu wa kilometa 200 kwa ajili ya wakandarasi wazawa hapa nchini.

Aidha, jumla ya kilometa 20 za barabara zimetengwa kwa ajili ya makandarasi wanawake ambapo zitagawanywa katika vipande vya kilometa tano tano na kazi hizo zitashindanishwa kwa makampuni ya wanawake peke yao.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mhandisi Mkuu kutoka Wizara ya Ujenzi Eng. Mtemi Simeon, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi wakati akifungua kongamano la tatu na maonesho ya wabunifu ya Wanafunzi wa. Uhandisi.

Eng. Simeon amesema kuwa nchi zote duniani ambazo zimepiga hatua kubwa za maendeleo zimekuwa zikitumia wataalam wake wa ndani katika kujenga uchumi wao hivyo kuna umuhimu mkubwa wa wahandisi wa ndani kuimarisha makampuni yao ya ushauri na uzalishaji, ili yawe na uwezo wa kushindana na yale ya nje, na pale inapobidi yaungane ili kuongeza nguvu na utaalamu.

"Ili wahandisi wawe bora ni lazima wapatiwe misingi na miongozo bora kuanzia ngazi ya uanafunzi ili nidhamu na uadilifu uwepo katika utekelezaji wa miradi mingi hapa nchini", amesisitiza Eng. Simeon.

Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, anathamini mchango wa wahandisi hapa nchini na amewapongeza kwa ubunifu mkubwa, ambao wanaonyesha

katika miradi ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutelelezwa.

"Katika moja ya vipaumbele na maagizo ya Mheshimiwa Rais katika sekta hii ni kuona ushiriki mkubwa zaidi wa makandarasi

wa ndani katika kazi za ujenzi wa miradi (Local Content)", amesema Eng. Simeon.

Ameeleza kuwa Serikali imefanya marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa kuongeza kiwango cha thamani ya mradi ambayo itatekelezwa na makandarasi wa ndani tu bila kushindanishwa na

makandarasi wa nje kutoka Shilingi bilioni10 iliyokuwepo zamani hadi Shilingi bilioni 50.

Naye Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania Eng. Dkt. Gemma Modu, ameeleza kuwa kongamano hilo ni fursa ya kuhamasisha na kuhimiza vijana kuingia kwenye uhandisi na kujikita kwenye ubunifu.

Pia kongamano hilo litakuza viwango na uwezo wa ubunifu wa kisayansi ili kuweza kuendana na kukidhi matakwa ya maendeleo ya teknolojia na ujuzi wa Karne ya 21.

Ametoa pongezi kwa Mhe. Rais kwa kasi ya utelelezaji wa miradi ya maendeleo na msisitizo wa mazingira rafiki ya kushirikisha wahandisi wazalendo na kuvutia uwekezaji.

Kongamano hilo lenye maudhui isemayo"Mchango wa Wahandisi Vijana katika ubunifu kwa Maendeleo Endelevu" limeandaliwa na Kitengo cha Wahandisi Vijana (Young Engineers) na Kitengo cha Wanafunzi (Students Chapter) Ngazi ya Taifa na kuhudhuriwa na wanafunzi kutoka Shule za Sekondari na Vyuo Vikuu.