Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

UKARABATI MV. MAGOGONI WAFIKA ASILIMIA 40


Ukarabati wa kivuko cha MV. Magogoni kilichokuwa kinatoa huduma kati ya Magogoni kuelekea Kigamboni jijini Dar es Salaam unaendelea huko mjini Mombasa nchini Kenya ambapo kwa sasa umefika asilimia 40.

Hayo yamebainishwa Januari 28, 2024 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa ajili ya kuwapa taarifa kuhusu maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho pamoja na mipango ya muda mrefu na mfupi na mikakati ya Wakala huo katika kuhakikisha huduma za vivuko katika eneo la Magogoni - Kigamboni na maeneo mengine yote Nchini unaimarika.

Kilahala amesema kuwa Wakala una mipango ya namna mbili ambayo ni ya muda mfupi na ya muda mrefu huku akitanabaisha kuwa mipango ya muda mfupi ni pamoja na kukodi Sea Taxi, vivuko vidogo viwili kutoka kampuni ya Bakhresa ambavyo vinaendelea kusaidiana na vivuko vilivyobakia katika eneo la Magogoni - Kigamboni kutoa huduma kwa wakazi wa maeneo hayo.

Kilahala ameongeza kuwa Mpango wa muda mrefu uliopo ni kuhakikisha kivuko cha MV. MAGOGONI kinamalizika kufanyiwa ukarabati mkubwa na kurejea kutoa huduma kwa haraka zaidi.

''Tunafahamu kwamba huu mradi umechukuwa muda mrefu zaidi ya tulivyotarajia, kulikuwa na changamoto za hapa na pale za kiutendaji lakini tunashukuru kwamba zimekwishatatuliwa, sasa hivi hiki kivuko kiko kwenye ukarabati na kimefika wastani wa asilimia 40”, amesema Mtendaji Mkuu

Aidha, Kilahala amesema kuwa TEMESA kwa sasa inataka kuongeza nguvu kwakuwa changamoto zote sasa zimekwishaanza kutatuliwa ili kuhakikisha ukarabati huo unakamilika kwa wakati na kuondoa kero iliyokuwepo.

Mtendaji Mkuu amesema kwakuwa vivuko MV. Kazi na Sea Taxi kwa sasa vinafanya kazi peke yake na haviwezi kutoa huduma ya uhakika, kutokana na sababu hiyo, Serikali inafanya mikakati ya makusudi kuhakikisha kivuko MV. KIGAMBONI kinafanyiwa ukarabati mdogo wa mara kwa mara ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma ya uhakika wakati wakisubiri kivuko MV. MAGOGONI kukamilika na kurejea kutoa huduma.

Kilahala amefafanua kuwa Serikali imeanza mchakato wa kutengeneza Sea Taxi nyingine mbili ambazo zitaenda kutoa huduma katika eneo hilo ili kurahisisha huduma ya usafiri.

Naye Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe, akizungumzia kuhusu kivuko MV. Kigamboni ambacho kimesimama kutoa huduma kutokana na kuharibika kwa mfumo wake wa uendeshaji, amesema tayari wameagiza vipuri ambavyo vinatarajiwa kuwasili kuanzia Tarehe 30 Januari, 2024.

‘’Vipuri vimetumwa kwa njia ya ndege kutoka Uholanzi na ni vipuri kwa ajili ya mfumo wa uendeshaji wa kivuko chetu cha MV. Kigamboni, kwahiyo vipuri vitakapofika mara moja timu yangu ya ufundi itafunga vipuri hivi na tunaamini hatuwezi kuchukua zaidi ya wiki kivuko kitarudi kwenye utendaji wake na tutawaita wenzetu wa TASAC kwa ajili ya kukikagua na kukiruhusu kiendelee kutoa huduma”, amesema Mhandisi King’ombe.