Habari
UKARABATI BARABARA YA KIA UKAMILIKE MACHI- KASEKENYA
Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi Rocktronic anayejenga barabara Njiapanda ya KIA kwenda KIA Km 5.7 Kuijenga barabara hiyo kwa ubora wa kimataifa na kuikamilisha ndani ya siku 200.
Akikagua maendeleo ya ujenzi huo leo, Eng. Kasekenya amesema barabara hiyo ni muhimu kwani ndio lango la kuingilia miji ya Arusha na Moshi hivyo ujenzi wake uwe sehemu ya utalii wa kanda ya Kaskazini.
"Serikali imeamua kuiboresha barabara hii ambayo itatumika kupitisha wageni wengi wakati wa mashindano ya AFCON hivyo ikamilike mapema zaidi na iwe na alama muhimu za barabarani, taa na njia ya watembea kwa miguu", amesisitiza Eng. Kasekenya.
Kwa upande wake Eng. Godlisten Nasario anayesimamia ujenzi huo amesema wamejipanga kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na ubora uliokusudiwa.
