Habari
UJENZI WA DARAJA LA PANGANI WAFIKIA ASILIMIA 72
📌 Mradi wenye thamani ya Sh bilioni 124.6 waendelea kutekelezwa mkoani Tanga.
Ujenzi wa Daraja la Pangani mkoani Tanga umefikia asilimia 72 ya utekelezaji wake, huku kazi zikiendelea katika hatua ya ujenzi wa sehemu ya juu ya daraja hilo.
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Kosani Msama, amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa Daraja la Pangani pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa jumla ya kilomita 25.6 katika kipande cha barabara ya Pangani–Tungamaa.
Amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Shandong Limited kutoka China kwa gharama ya Sh bilioni 124.6, chini ya usimamizi wa kampuni ya Lea kutoka India, huku ufadhili ukitolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi huo, Mhandisi Msama amesema kazi za msingi pamoja na ujenzi wa nguzo zote tisa za daraja hilo zimekamilika, huku ujenzi wa sehemu ya juu ya daraja (deck) ukiendelea kwa kutumia teknolojia ya Moving Scaffolding System (MSS).
Amesema teknolojia hiyo ni miongoni mwa mifumo inayotumika katika ujenzi wa madaraja, ikisaidia utekelezaji wa kazi za sehemu ya juu ya daraja kwa kutumia vifaa maalumu vya kisasa.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kupunguza utegemezi wa vivuko, kuongeza fursa za biashara na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, hususan kwa wananchi wa Pangani, mkoa wa Tanga na maeneo mengine.
Mhandisi Msama ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo, huku akitoa shukrani kwa Wizara ya Ujenzi na uongozi wa TANROADS kwa ushirikiano na usimamizi wa mradi.
