Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

TANROADS YATOA MAFUNZO KWA WAAJIRIWA WAPYA.


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amefungua mafunzo ya siku kumi ya Wahandisi wapya walioajiriwa na Serikali kupitia TANROADS wapatao 49 ambao watapelekwa kufanya kazi sehemu mbalimbali Nchini ili kupunguza uhaba wa watumishi wa kada hiyo katika sekta ya Ujenzi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufungua mafunzo hayo yaliyoanza leo tarehe 30 Oktoba 2023 katika Ukumbi wa Kobe Sabasaba Jijini Dar- es Salaam Mhandisi Besta amesema ni muendelezo wa hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa na Serikali kuwawezesha na kuwaongezea uwezo wa kitaaluma Wahandisi ili waweze kusimamia vizuri kazi za ujenzi wa miundombinu ya barabara na Madaraja.

Ameeleza “Mafunzo haya yamefanyika kuwaongezea chachu na kupata Wahandisi wapya wenye ueledi lengo ni kuimarisha utendaji kazi hasa katika usimamizi wa viwango katika ujenzi wa barabara hivyo nachukua fursa hii kumshukuru Rais wetu  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Ujenzi na Serikali kwa ujumla kwa kutoa kibali kwa TANROADS kuajiri Wahandisi wapya kabisa ambao wataenda kuongeza ufanisi hasa katika maeneo ambayo Wahandisi wametoka kwa kustaafu ama kuhamia maeneo mengine".

“Lazima tuwajenge Wahandishi wapya  ninawataka wafahamu kwamba wanaenda kuhudumia miundombinu ya takribani Kilomita 36,760 nchi nzima pamoja na miradi mingi inayoongezeka sio katika ngazi ya Kitaifa tu lakini vilevile katika ngazi ya Mikoa kwa hiyo baada ya mafunzo haya nina amini watakuwa wamejiweza, tutaendelea kuwasimamia na kutoa mafunzo ya namna hii mara kwa mara ili kuendelea kuwajengea uwezo kwa jinsi ambavyo teknolojia inavyoendelea kubadilika’’.

Naye Meneja Rasilimali watu na Utawala wa TANROADS Bw. Pilika Kasanda amesema watumishi hao wapya ambao wameajiriwa kuanzia mwezi wa 10 mwaka huu 2023 ni muendelezo wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameridhia TANROADS kuajiri jumla ya watumishi 125 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hususani miradi mipya ambayo inaendelea kutekelezwa na Serikali ikiwemo ile ya EPC + F.

Ameongeza kuwa “Mhe Rais Dkt. Samia ametoa kibali waajiriwe Wahandisi 63 na Mafundi 62 jumla 125; katika kibali hicho awamu ya kwanza tumepata Wahandisi 49 ambao wameanza kufanyiwa taratibu za awali za ajira, tulianza na mafunzo ya utayari wa kuajiriwa kwenye utumishi wa Umma na leo tumeendelea na mafunzo ya Kitaaluma ambayo yametolewa na wakufunzi wetu wa ndani lengo ni kuwawezesha na kuwajengea uwezo Wahandisi hawa wapya kabla ya kwenda kufanya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya Mikoa ya Tanzania bara.