Habari
TANROADS watakiwa kutumia mtambo wa kupima Barabara

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameutaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kutumia mtambo wa kupima ubora wa barabara (Road scanner) ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa ubora unaotakiwa kabla ya kukamilika kwa mradi na kukabidhiwa Serikalini.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua mradi wa upanuzi wa barabara ya Morogoro sehemu ya Kimara - Kibaha (Km19.2), kuwa njia nane na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili mkoani Dar es Salaam.
Amesema kuwa licha ya mtambo huo kuwezesha kutambua ubora wa barabara pia unasaidia kutambua mapungufu yaliyopo kwenye miradi ya ujenzi kabla ya kukamilika na kukabidhiwa.
"Naelewa kuwa mtambo huo upo Wizarani na ninaagiza TANROADS kukamilisha taratibu zote na kuanza kutumia teknolojia hii kurahisisha ukaguzi na kuondokana na njia ya zamani ya kukata vipande vya lami njia ambayo haileti matokeo sahihi", amesema Mbarawa.
Aidha, Waziri Mbarawa ameutaka Wakala huo kuhakikisha wanawasimamia vema makandarasi katika hatua za awali za ujenzi na wakati ujenzi unaendelea na kutowapa kazi wale wote ambao wanajenga chini ya viwango kwani serikali inatumia gharama kubwa katika ujenzi wa miundombinu hiyo.
Aidha, Profesa Mbarawa ameridhishwa na utekelezaji wa mradi wa barabara ya Kimara hadi Kibaha na kuwataka TANROADS kukamilisha makubaliano na mkandarasi mapema ili waweze kukamilisha asilimia iliyobakia kulingana na makubaliano.
Vilevile Waziri huyo amemtaka mkandarasi anayejenga miundombinu ya mabasi yaendayo haraka kuhakikisha anajenga kwa viwango na kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa katika barabara hiyo kwa kufumua na kujenga upya eneo la kilomita mbili sehemu ya Mbagala ambapo kuna hitilafu zilizojitokeza.
Awali akitoa taarifa ya mradi wa Kimara - Kibaha, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Rogatus Mativila, amemhakikishia Waziri huyo kuwa watahakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati na kusimamia mapungufu yaliyobainishwa na Waziri huyo.
Mhandisi Mativila amesema kuwa mkandarasi amemaliza usanifu wa mradi huo kwa asilimia 94 ikiwa ni ujenzi wa njia sita mpya (tatu kila upande) zenye urefu wa kilometa 19.2 na upana wa mita 9 kila upande.
Kazi nyingine ni ujenzi wa njia za maingilio, njia za watembea kwa miguu, makutano yenye taa, ujenzi wa madaraja sita, ujenzi wa daraja la juu Kibamba CCM, ujenzi wa daraja la wavuka kwa miguu mbezi mwisho, pamoja na miundombinu ya maji ya mvua.