Habari
SERIKALI YAJA NA MPANGO WA KUMALIZA FOLENI KWENYE MIZANI NCHINI.
Serikali inatarajia kutenga Shilingi bilioni 81 kwa ajili ya ujenzi wa mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion) kote nchini ili kuondoa msongamano na kupunguza muda wa kupima magari.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hayo wilayani Bunda mkoani Mara wakati akikagua mradi wa ujenzi wa mzani wa kupima magari wa Rubana.
"Katibu Mkuu (ujenzi), tathmini tuliyoifanya ya kubadilisha mizani yote nchini kwenye miaka mitatu ijayo ya bajeti kuanzia mwaka 2024/25 tuweke bajeti kwa awamu, hiyo bajeti ya Shilingi bilioni 81 tuigawe kwa tatu ili kila mwaka tuwe na kiasi cha fedha kwa ajili ya utekelezaji," alisema Waziri Bashungwa.
Waziri amesema lengo la serikali ni kuhakikisha mizani yote nchini ambayo haina iwezo wa kupima Magari yakiwa kwenye mwendo inakuwa ni ya kisasa, kwamba tathimini ya gharama ya utekelezaji imeshafanyika.
"Hivi sasa tunajua kwamba mizani yote nchini ili iwe na weigh in motion ambayo gari haliitaji kupanga foleni ili kujua limebeba uzito kiasi gani tathimini tuliyoifanya tunahitaji kuweka kwenye mizani yote nchini kwa gharama ya Shilingi bilioni 81," alisema Bashungwa.
Amesema faida ya kuweka mizani hiyo, itarahisisha mzunguko wa huduma na usafirishaji pasipo kuchelewesha wasafirishaji kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Aidha, Bashungwa amewataka watumiaji wa barabara nchini kutozidisha uzito katika magari ili kulinda barabara zidumu kwa miaka mingi zaidi."Wadau wa usafirishaji tuzingatie sheria za usalama barabarani, sheria ya uzito wa magari yanayoruhusiwa kupita kwenye barabara zetu," alisema Waziri Bashungwa.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi unaoendelea kwenye mradi wa ujenzi wa mzani wa kupima magari wa Rubana, Meneja wa Mizani kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Eng. Leonard Mombia alisema kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 77.
Ameeleza kuwa mzani huu ni wa kwanza utakaofungwa scanner kwa ajili ya kuchukua vipimo vya ukubwa wa magari na mizigo iliyobebwa.
Kukamilika kwa ujenzi wa Mzani huo kutasaidia kuondoa msongamano kwani utapima magari kwa kutumia muda mfupi na pia kutasaidia kudhibiti uzito wa magari na mizigo isiyokuwa ya kawaida (Abnormal Loads) inayohatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.