Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

SERIKALI KUIFUNGUA WILAYA YA RUNGWE KWA BARABARA ZA LAMI


Serikali imesema inaenda kumaliza kero ya wananchi wa wilaya ya Rungwe kwa kuikamilisha ujenzi wa barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu (km 79.4) sehemu ya Katumba- Lupaso (km 35.3) na Mbaka - Kibanja (km 20.7) kwa kiwango cha lami ili kuchochea shughuli za biashara na kukuza uchumi.

Aidha, barabara hizo ni za kimkakati kwani zinapitia maeneo yenye shughuli nyingi za kilimo, ufugaji na biashara na inaunganisha wananchi wa Wilaya ya Rungwe na Tukuyu hivyo kukamilika kwake kutarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao na chakula.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, Oktoba 1, 2023 katika kijiji cha Kandete, Halmashauri ya Busokelo mkoani Mbeya wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara mkoani humo. Bashungwa ameambatana na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba  ambapo  wameikagua barabara hiyo ambayo ni maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa mkoa huo.

Bashungwa ameeleza katika barabara hiyo Serikali imeshatumia Bilioni 21.307 kwa kuijenga kwa kiwango cha lami sehemu ya kwanza inayoanzia Bujesi - Mbambo (km 12.7), na Sehemu ya pili inayoanzia Kibanja - Tukuyu (km 7) na mkandarasi kutoka kampuni ya kichina ya China Railway 15 Group kwa muda wa miezi 45.

Bashungwa ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wa uzalishaji unaofanywa na wilaya hizo ameridhia barabara hiyo iendelee kukamilishwa kwa kiwamgo cha lami sehemu ya tatu kuanzia Katumba- Lupaso (km 35.3) na sehemu ya nne inayoanzia Mbaka - Kibanja (km 20.7) kwa kiwango cha lami.

"Mhe. Rais anafahamu barabara hii na ameridhia iwekwe lami na hivi karibuni tunakwemda kutia saini mkataba wa ujenzi na tutamwalika Mhe. Mbunge wa jimbo la Busokelo kuja kushuhudia mkoani Dodoma", amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Mbeya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa kilometa 9 wa barabara inayounganisha na Wilaya ya Makete mkoani Njombe na kuifungua barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ili wananchi waweze kupata huduma za kijamii kwa urahisi.

Waziri Bashungwa ameagiza pia kiasi cha shilingi Milioni 231 za fidia kwa wananchi ziweze kulipwa kwa walipisha mradi huo. Bashungwa amesema ujenzi wa barabara hiyo utagharamiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa kapu la mama lipo salama na amejionea mwenyewe hali ya barabara hivyo anasubiria maombi ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ili kazi za ujenzi wa barabara hiyo uanze na kukamilika kwa haraka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ameeleza kuwa mkoa umekwishatekeleza agizo la Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuunganisha makao makuu ya wilaya zote kwa taa za barabarani ili wananchi waweze kufanya biashara usiku na mchana.

Homera amewashukuru Mawaziri hao kwa umoja wao  kwa kufika mkoani humo na kumsaidia Mhe. Rais katika kusukuma kazi za miradi zinazoendelea kutekelezwa na kuufungua mkoa huo kiuchumi.

Akitoa taarifa ya mradi Mkurugenzi wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Boniface Mkumbo ameeleza kuwa utelelezaji wa mradi huo sehemu ya kwanza na pili umefikia asilimia 98 na kazi zilizobakia ni kuweka alama za barabarani pamoja na taa za barabarani.

Eng. Mkumbo amesema barabara hiyo kwa sasa ipo katika kipindi cha matazamio kwa kipindi cha mwaka mmoja na kitaisha tarehe 14/06/2024.