Habari
ONGEZENI SPIDI UJENZI BRT III - PROF. MBARAWA
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi SINOHYDRO Corporation Ltd anayejenga barabara ya Usafiri wa Haraka wa Mabasi BRT III kutoka katikati ya jiji la Dar es Salaam hadi Gongolamboto KM 23.3 kuongeza spidi ili kukamilisha kazi hiyo ifikapo Mei mwakani.
Amesema ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni ya kiuchumi na lango la kuingilia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam unastahili kujengwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu na kukamilika kwa wakati ili kuleta tija iliyokusudiwa.
"...Hakikisheni mnafanya kazi kwa saa 24 pale inapowezekana na kusimamia vizuri magari yanayotumia barabara hii ili kupunguza msongamano na kulinda usalama wa watumiaji wa barabara," amesema Waziri Mbarawa.
Prof. Mbarawa amezungumzia umuhimu wa mkandarasi na TANROADS kushirikiana kikamilifu kuhakikisha barabara hiyo muhimu na ya kimkakati inapitika wakati wote ikiwa salama ili kutowakwaza watumiaji wa barabara hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Mohamed Besta amesema kazi ya ujenzi wa barabara hiyo imegawanywa katika sehemu mbili ambapo, sehemu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara KM 23.3, Vituo vya Mabasi 32, na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Gongo la Mboto wakati sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa karakana, Kituo Kikuu ndani ya eneo la Uwanja wa Ndege, na Kituo mlisho (feeder Station) eneo la Banana njia panda ya Kitunda.
Mhandisi Mshauri wa Mdaradi huo, Frank Mbilinyi amemhakikishia Mhe. Waziri wa Ujenzi kuwa wamejipanga kikamilifu kumsimamia Mkandarasi ili kupunguza msongamano wa magari na kuzingatia usalama wa watumiaji wa barabara katika kipindi ambacho ujenzi unaendelea.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Selemani ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa inaoufanya katika barabara hiyo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkandarasi kwa kutotupa takataka hovyo maeneo ya ujenzi.
Zaidi ya shilingi bilioni 231 zinatarajiwa kutumika katika mradi huo unaotarajiwa kukamilika baadaye mwakani ikiwa ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuboresha huduma za usafiri jijini Dar es salam ambapo tayari awamu ya kwanza ya BRT toka katikati ya jiji kwenda Kimara na Magomeni hadi Morocco KM 20.9 imekamilika huku awamu ya pili ya BRT KM 20.3 toka katikati ya jiji hadi Mbagala ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 96 kukamilika.
Prof. Mbarawa yuko jijini Dar es Salaam kwenye ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu mbalimbali hususan maendeleo ya mfumo wa usafiri wa haraka wa mabasi ya BRT.